• HABARI MPYA

    Sunday, May 20, 2018

    ASANTE MUHESHIMIWA RAIS DK. MAGUFULI, MIAKA MIWILI YATOSHA KUWA KIPIMO CHAO!

    RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Joseph Magufuli jana alijumuika na maelfu ya mashabiki wa soka, wengi wao wapenzi wa Simba SC kutazama mchezo wa Ligi Kuu baina ya klabu hiyo na Kagera Sugar ya Bukoba Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
    Rais Magufuli alifika uwanjani mapema tu Saa 8:00 mchana na akapata fursa ya kusalimiana na wachezaji wa timu zote mbili kabla ya kwenda jukwaani kuushuhudia mchezo huo, ambao mwishowe wenyeji Simba walichapwa 1-0, bao pekee la mchezaji wao wenyewe wa zamani, Edward Christopher Shijja dakika za mwishoni.   
    Na kama ilivyotarajiwa, Rais Magufuli baada ya mchezo akazungumza kuwahutubia maelfu waliojitokeza uwanjani na mamilioni wengine waliokuwa wanafuatilia matangazo ya moja kwa moja kupitia Televisheni ya Azam.
    Katika hotuba yake fupi, Rais Magufuli alisema kwamba inatosha sasa kwa timu za Tanzania kufungwa kwenye mashindano ya kimataifa baada ya kufungwa kwa muda mrefu tangu Uhuru mwaka 1961.

    Rais Magufuli alisema ni miaka mingi sasa tangu taifa limepata uhuru, lakini timu za nchini zimekuwa hazifiki mbali kwenye mashindano ya kimataifa na akasema ufike wakati timu zetu ziweze kushiriki Kombe la Afrika na kombe la Dunia.
    Rais alisema amekuwa haiingii kwenye viwanja vya mpira kwa sababu ya maudhi ya timu zetu kushindwa. “ifike mahali tuanze kushinda, tumeshindwa vya kutosha. Ifike mahali sasa tushinde. Viongozi wa TFF, BMT na klabu tuweke mikakati ya ushindi. Ni aibu kubwa, tumesindwa vya kutosha,”alisema Rais Magufuli ambaye pia jana aliwakabidhi Kombe la ubingwa wa Ligi Kuu Simba.
    “Mimi sina timu, napenda michezo, napenda michezo timu zangu za Tanzania zishinde. Simba mkichukua Kombe nitakuja, Yanga ikichukua Kombe nitakuja, hata Kagera mkichukua kombe nitakuja. Huo ndiyo wito wagu,” alisema Rais Magufuli ambaye pia aliwaomba Simba wakawe timu ya kwanza kuleta Kombe la Afrika.
    Pamoja na hayo, Rais Magufuli aliwaambia Simba SC wakaboreshe uwezo wao kuelekea kwenye michuano ya Afrika mwakani; “Nimewaheshimu nimekuja hapa kuwapa Kombe, ninawaomba sana mkabadilishe mchezo, mpira wa leo niliouona hamuwezi kuchukua Kombe la Afrika. Ni lazima tubadilike. Mimi ni shabiki wa Taifa Stars, Kagera Sugar mmecheza mchezo mzuri sana, kwa Simba mmejitahidi kudhihirisha ni washindi, mmechukua Kombe,”alisema. 
    Rais Magufuli pia aliwapongeza Serengeti Boys kwa ushindi wa Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge akasema anaamimi watabakiza na Kombe la Mataifa ya Afrika, michuano ambayo itafanyika nyumbani Aprili mwakani.
    Akaipongeza timu ya watoto wa mitaani ya Tanzania kwa kushika nafasi ya pili kwenye michuano ya Kombe la Dunia ya Watoto Wanaoishi kwenye Mazingira Magumu nchini Urusi baada ya kufungwa na Brazil kwenye fainali.
    Akawataka viongozi wa klabu na TFF kuibua vipaji na kuviendeleza, kwa sababu kwa muda mrefu kumekuwa na desturi ya kuibua vipaji, lakini haviendelezwi.
    Rais Magufuli akasema Serikali itaendelea kutoa mafunzo, kuajiri wataalamu na watashirikiana bega kwa began a TFF katika maandalizi ya AFCON U-17 ikiwa ni pamoja na kuiandaa Serengeti Boys ili Kombe libaki nyumbani an kuepukana na desturi ya kuwa kichwa cha mwendawazimu.
    Rais pia akazungumzia ujenzi wa Uwanja wa kisasa mjini Dodoma kwa msaada wa Serikali ya Morocco na kuwataka wanamichezo watunze miundombinu. “Tukio kama lile la kuvunja viti halipaswi kujirudia. Nakiagiza na chama changu, CCM nacho kiboreshe viwanja vyake na Halmashauri zote zitenge maeneo ya michezo. Tukifanya hivi michezo itakuwa,”alisema.
    Rais Magufuli akasema akasema anaambiwa na Yanga wanashiriki Kombe la Shirikisho, nao akawataka washinde, kwa sababu yeye anataka timu inayoshinda.
    Hotuba ya Rais Magufuli jana imebeba ujumbe mzito wa kufanyia kazi kwa viongozi wetu wa michezo nchini na inapaswa iwe kipimo chao kwa miaka miwili ijayo – vinginevyo watakuwa wametuthibitishia wameshindwa.
    Mezani tuna timu mbili zinazowania tiketi ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika ambazo ni ya vijana chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro Heroes na ya wakubwa, Taifa Stars baada ya timu ya wanawake, Twiga Stars kutolewa na Zambia.   
    Kwa sababu tutakuwa wenyeji wa AFCON U17 mwakani, Serengeti Boys itashiriki moja kwa moja mashindano hayo – lakini timu nyingine mbili Ngorongoro Heroes na Taifa Stars zitalazimika kupigana kwa jasho kuwania tiketi ya fainali za Afrika.
    Ngorongoro leo inateremka Uwanja wa Omnisports Modibo Keita mjini Bamako, kumenyana na wenyeji, Mali katika mchezo wa marudiano Raundi ya pili ya mchujo wa kuwania tiketi ya Fainali za U20 mwakani nchini Niger, ikitakiwa kushinda kuanzia mabao 2-0 ugenini ili kusonga mbele, kufuatia kukubali kipigo cha mabao 2-1 kwenye mchezo wa kwanza Mei 13 Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
    Taifa Stars kuelekea fainali za AFCON za mwakani nchini Cameroon ipo Kundi L pamoja na Uganda, Lesotho na Cape Verde na hadi sasa kila timu imecheza mechi moja tu, The Cranes pekee wakivuna pointi tatu kwa ushindi wa 1-0 ugenini dhidi ya Papa wa Bluu huku Tanzania wakilazimishwa sare ya 1-1 na Mamba. 
    Mechi tano zijazo ni nyingi na ndizo zitaamua hatima ya Taifa Stars katika kinyang’anyiro cha tiketi ya AFCON ya pili kihistoria baada ya ile ya mwaka 1980 nchini Nigeria – na ndiyo maana ninasema miaka miwili ijayo yatosha kuwa kipimo cha uongozi wa sasa wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kwa sababu hata Rais amesema ifike wakati twende AFCON na Kombe la Dunia baada ya kufungwa kwa muda mrefu. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: ASANTE MUHESHIMIWA RAIS DK. MAGUFULI, MIAKA MIWILI YATOSHA KUWA KIPIMO CHAO! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top