• HABARI MPYA

    Saturday, July 09, 2016

    JUMA ABDUL, TSHABALALA NA KICHUTA 'WABANANISHWA' TUZO YA MCHEZAJI BORA LIGI KUU

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KIUNGO wa Mtibwa Sugar ya Morogoro, Shizza Ramadhani Kichuya atachuana na mabeki Juma Abdul Jaffar wa Yanga na Mohammed Hussein 'Tshabalala' wa Simba kuwania tuzo ya Mchezaji Bora wa Msimu wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Katika taarifa ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa vyombo vya Habari leo, walinda milango Aishi Manula wa Azam FC, Beno Kakolanya wa Prisons na Deogratius Munishi wa Yanga watachuana kuwania tuzo ya kipa bora.
    Tuzo ya Kocha bora inawaniwa na Mholanzi Hans van Pluijm wa Yanga, Mecky Maxime wa Mtibwa Sugar na Salum Mayanga wa Prisons, wakati tuzo ya Mchezaji Bora Chipukizi inawaniwa na Farid Mussa wa Azam FC, Tshabalala wa Simba, Muzamil Yassin wa Mtibwa Sugar na Kichuya.
    Beki wa Yanga, Juma Abdul akimdhibiti kiungo wa Azam FC, Farid Mussa katika mchezo wa Ligi Kuu
    Tuzo ya Mchezaji Bora wa Kigeni inawaniwa na Wazimbabwe kiungo Thabani Kamusoko na mshambuliaji Donald Ngoma wote wa Yanga watakaochuana na kipa Muvory Coast wa Simba, Vincent Agban, wakati Anthony Kayombo, Ngole Mwangole na Rajab Mrope watachuana katika tuzo ya Refa Bora.
    Sherehe za kukabidhi tuzo za washindi zitafanyika Julai 17 mwaka huu mjini Dar es Salaam katika zoezi linalodhaminiwa na Vodacom Tanzania na kuratibiwa na Kamati ya Tuzo ya TFF, inayoundwa na waandishi wa habari za michezo, makocha, viongozi na wawakilishi wa wadhamini, Vodacom na Azam TV.
    Katika usiku huo, pia mabingwa Yanga, washindi wa pili, Azam FC, washindi wa tatu, SImba SC, washindi wa nne, Prisons na timu yenye nidhamu watakabidhiwa zawadi zao sambamba na mfungaji bora, Amissi Tambwe wa Yanga.
    Meneja Uhusiano wa Vodacom Tanzania, Matina Nkurlu amewapongeza wateule wote waliopendekezwa kuwania tuzo hizo. "Kama wadhamini tuna matumaini makubwa kuwa msisimko wa ligi hii utazidi kuongezeka katika msimu ujao na kuzidi kuwapatia mashabiki wa soka wanaoifuatilia hapa nchini na nje ya nchi."
    Alisema Vodacom itaendelea kudhamini ligi hiyo kubwa ya soka nchini  ili kutekeleza moja ya malengo yao ya kuibua na kuendeleza vipaji vya wachezaji nchini. Pia kuwawezesha wachezaji kujipatia ajira na kuboresha maisha yao kupitia sekta ya michezo bila kusahau kuwapatia burudani wateja wake na Watanzania wote kwa ujumla.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: JUMA ABDUL, TSHABALALA NA KICHUTA 'WABANANISHWA' TUZO YA MCHEZAJI BORA LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top