• HABARI MPYA

  Sunday, May 20, 2018

  MAGUFULI: TUMEFUNGWA VYA KUTOSHA, IMEFIKA WAKATI TUANZE KUSHINDA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM 
  RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Joseph Magufuli amesema kwamba Tanzania imefungwa vya kutosha kwenye mashindano ya kimataifa ya soka na umefika wakati ianze kushinda. 
  Rais Magufuli aliyasema hayo jana jioni Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam baada ya mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kati ya Simba SC na Kagera Sugar. 
   Rais Magufuli alisema ni miaka mingi sasa tangu taifa limepata uhuru mwaka 1961, lakini timu za nchini zimekuwa hazifiki mbali kwenye mashindano na akaagiza ufike wakati timu zetu ziweze kushiriki Kombe la Afrika na kombe la Dunia. 
  “Sijawahi kuingia kwenye mpira wowote kwa sababu ya frustration ya timu zetu kushindwa. Ifike mahali tuanze kushinda, tumeshindwa vya kutosha. Ifike mahali sasa tushinde. 
  Viongozi wa TFF, BMT na klabu tuweke mikakati ya ushindi. Ni aibu kubwa, tumesindwa vya kutosha,”alisema Rais Magufuli ambaye pia jana aliwakabidhi Kombe la ubingwa wa Ligi Kuu Simba.

  “Mimi sina timu, napenda michezo, napenda michezo timu zangu za Tanzania zishinde. Simba mkichukua Kombe nitakuja, Yanga ikichukua Kombe nitakuja, hata Kagera mkichukua kombe nitakuja. Huo ndiyo wito wagu,” alisema Rais Magufuli ambaye pia aliwaomba Simba wakawe timu ya kwanza kuleta Kombe la Afrika. 
  Pamoja na hayo, Rais Magufuli aliwaambia Simba SC wakaboreshe uwezo wao kuelekea kwenye michuano ya Afrika mwakani; “Nimewaheshimu nimekuja hapa kuwapa Kombe, ninawaomba sana mkabadilishe mchezo, mpira wa leo niliouona hamuwezi kuchukua Kombe la Afrika. Ni lazima tubadilike. Mimi ni shabiki wa Taifa Stars, Kagera Sugar mmecheza mchezo mzuri sana, kwa Simba mmejitahidi kudhihirisha ni washindi, mmechukua Kombe,”alisema. 
  Rais Magufuli pia aliwapongeza Serengeti Boys kwa ushindi wa Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge akasema anaamimi watabakiza na Kombe la Mataifa ya Afrika, michuano ambayo itafanyika nyumbani Aprili mwakani. 
  Akaipongeza timu ya watoto wa mitaani ya Tanzania kwa kushika nafasi ya pili kwenye michuano ya Kombe la Dunia ya Watoto Wanaoishi kwenye Mazingira Magumu nchini Urusi baada ya kufungwa na Brazil kwenye fainali. 
  Akawataka viongozi wa klabu na TFF kuibua vipaji na kuviendeleza, kwa sababu kwa muda mrefu kumekuwa na desturi ya kuibua vipaji, lakini haviendelezwi. 
  Rais Magufuli akasema Serikali itaendelea kutoa mafunzo, kuajiri wataalamu na watashirikiana bega kwa began a TFF katika maandalizi ya AFCON U-17 ikiwa ni pamoja na kuiandaa Serengeti Boys ili Kombe libaki nyumbani an kuepukana na desturi ya kuwa kichwa cha mwendawazimu. 
  Rais pia akazungumzia ujenzi wa Uwanja wa kisasa mjini Dodoma kwa msaada wa Serikali ya Morocco na kuwataka wanamichezo watunze miundombinu. 
  “Tukio kama lile la kuvunja viti halipaswi kujirudia. Nakiagiza na chama changu, CCM nacho kiboreshe viwanja vyake na Halmashauri zote zitenge maeneo ya michezo. 
  Tukifanya hivi michezo itakuwa,”alisema. Rais Magufuli akasema akasema anaambiwa na Yanga wanashiriki Kombe la Shirikisho, nao akawataka washinde, kwa sababu yeye anataka timu inayoshinda.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MAGUFULI: TUMEFUNGWA VYA KUTOSHA, IMEFIKA WAKATI TUANZE KUSHINDA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top