• HABARI MPYA

  Wednesday, May 16, 2018

  RAIS MAGUFULI AKUBALI KUWAKABIDHI SIMBA SC KOMBE JUMAMOSI…AWATAKIA KILA LA HERI YANGA MECHI NA RAYON LEO

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Joseph Magufuli amekubali kuwakabidhi Kombe la ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Simba SC Jumamosi Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Hayo yamesemwa mchana wa leo na Mtendaji Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wilfred Kidau alipozungumza na Waandishi wa Habari leo makao makuu ya ofisi za shirikisho, Uwanja wa Karume, Ilala mjini Dar es Salaam.
  Pamoja na hayo, Kidau amesema kwamba Rais Magufuli amewatakia kila la heri, Yanga SC katika mchezo wao wa leo Kundi D Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Rayon Sport ya Rwanda.
  Kidau amesema Rais Magufuli kabla ya kuwakabidhi Simba SC Kombe la ubingwa wa Ligi Kuu, ataanza kwa kukabidhiwa Kombe la ubingwa wa michuano ya Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 (CECAFA U17), ambalo Tanzania ilitwaa mapema mwezi huu nchini Burundi. 

  Rais Dk. John Pombe Joseph Magufuli amekubali kuwakabidhi Kombe Simba SC Jumamosi  

  Simba SC wanatarajiwa kuwaalika Kagera Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Mechi hiyo itakuwa maalum kwa Wekundu hao wa Msimbazi kukabidhiwa taji la ubingwa wa Ligi Kuu walilolitwaa Alhamisi wiki iliyopita baada ya mahasimu wao wa jadi, Yanga SC kufungwa 2-0 na Tanzania Prisons mjini Mbeya.
  Simba SC wakajihakikishia wao ni mabingwa wa nchi baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Singida United Jumamosi Uwanja wa Namfua mjini Singida.
  Simba SC wamekwishajikusanyia pointi 68 hadi katika mechi 28, ambazo kati ya hizo wameshinda 20 na kutoa sare nane na baada ya mchezo wa Jumamosi watakwenda kukamilisha msimu kwa mchezo dhidi ya Maji Maji mjini Songea mkoani Ruvuma.
  Wakati huo huo: Yanga SC inateremka Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam Saa 1:00 usiku wa leo kumenyana na Rayon Sport ya Rwanda ktika mchezo wa Kundi D Kombe la Shirikisho Afrika.
  Yanga ilianza vibaya mechi za makundi Kombe la Shirikisho Mei 6 kwa kufungwa mabao 4-0 na wenyeji, U.S.M. Alger Uwanja wa Julai 5, 1962 mjini Algiers, Algeria wakati Rayon ililazimishwa sare ya 1-1 na Gor Mahia siku hiyo mjini Kigali.
  Michuano ya Kombe la Shirikisho itasimama baada ya mechi za katikati ya wiki hii, Yanga na Rayon na Gor Mahia na USM Alger kupisha Fainali za kombe la Dunia mwezi ujao nchini Urusi. Yanga watakamilisha mechi zao za mzunguko wa kwanza kwa kuwafuata Gor Mahia mjini Nairobi Julai 18.
  Mzunguko wa pili Yanga itaanzia nyumbani Julai 29 na Gor Mahia, kabla ya kuwakaribisha na USMA Alger Agosti 19 na kwenda kumalizia ugenini Agosti 29 na Rayon.
  Timu mbili za juu kutoka kila kundi katika makundi yote manne, zitakutana katika hatua ya Robo Fainali na baadaye Nusu Fainali itakayozaa Fainali. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: RAIS MAGUFULI AKUBALI KUWAKABIDHI SIMBA SC KOMBE JUMAMOSI…AWATAKIA KILA LA HERI YANGA MECHI NA RAYON LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top