• HABARI MPYA

    Wednesday, May 16, 2018

    MO DEWJI AKUBALI KUNUNUA ASILIMIA 49 SIMBA SC, MKUTANO WA KUPITISHA MABADILIKO YA KATIBA NI JUMAPILI

    Na Sada Salmin, DAR ES SALAAM
    MFANYABIASHARA Mohammed ‘Mo’ Dewji amekubali kununua asilimia 49 za hisa za klabu ya Simba SC kulingana na maelekezo ya Serikali.
    Hayo yamesemwa na Mwanasheria wa klabu ya Simba SC, Evodius Mtawala katika mkutano na Waandishi wa Habari uliofanyika hoteli ya Serena mjini Dar es Salaam leo.
    Mtawala amewataka wanachama wa Simba SC kujitokeza kwa wingi katika Mkutano wa mabadiliko ya Katiba utakaofanyika Mei 20, mwaka huu katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere uliopo eneo la Ocean Road mjini Dar es Salaam.
    Mkutano huo ulioitishwa na Kaimu Mwenyekiti, Salim Abdallah ‘Try Again’ utaanza Saa 3:00 asubuhi na tayari wanachama wamekwishasomewa ajenda kwa mujibu wa Ibara ya 22 ya klabu hiyo, kufungu cha nne.
    Mohammed ‘Mo’ Dewji amekubali kununua asilimia 49 Simba SC kulingana na maelekezo ya Serikali

    Mkutano huo utafuatia ule wa Desemba 3, mwaka jana, ambao uliazimia kumfanya mfanyabiashara Mohammed ‘Mo’ Dewji kuwa mwanahisa mkuu wa klabu katika mfumo mpya wa uendeshwaji wa Simba SC.
    Mo pekee aliweka dau la Sh Bilioni 20 kuomba asilimia 50 ya hisa, baada ya klabu kutangaza kuuza asilimia 50 ya hisa zake kwa Sh. Bilioni 20 miezi miwili iliyopita, ingawa baadaye Serikali ikaagiza klabu hiyo isiuze zaidi ya asilimia 49 kwa mtu mmoja.
    Wanachama 1320 walihudhuria mkutano huo wa Desemba kutoka Dar es Salaam na mikoa jirani na kwa furaha ya ushindi huo, Mo Dewji alitoa ahadi 10 za kuleta mabadiliko makubwa, ikiwemo ujenzi wa Uwanja wa mazoezi wa nyasi za asili na nyasi bandia pamoja na hosteli ya kisasa ya wachezaji.
    Wakati huo huo: Simba SC inaendelea na maandalizi ya sherehe za ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara huku wakisubiri majibu ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Joseph Magufuli aliyeombwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuhudhuria mchezo huo ili pia awakabidhi Kombe Simba.
    Simba SC wamekwishajikusanyia pointi 68 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine kuelekea mechi mbili za mwisho za msimu. Katika mechi 28 walizocheza hadi sasa, Simba wameshinda 20 na kutoa sare nane na baada ya mchezo wa Jumamosi watakwenda kukamilisha msimu kwa mchezo dhidi ya Maji Maji mjini Songea mkoani Ruvuma.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MO DEWJI AKUBALI KUNUNUA ASILIMIA 49 SIMBA SC, MKUTANO WA KUPITISHA MABADILIKO YA KATIBA NI JUMAPILI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top