• HABARI MPYA

    Friday, May 18, 2018

    MAHAKAMA KUU YAMKUBALIA WAMBURA KUZIFUNGULIA KESI KAMATI ZA TFF

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam imekubali maombi ya aliyekuwa Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Michael Richard Wambura ya kufanya marejeo dhidi ya maamuzi ya Kamati za shirikisho hilo.
    Hayo yamesemwa na Wakili maarufu katika mambo ya michezo nchini, Emmanuel Muga katika taarifa yake kwa vyombo vya Habari leo mjini Dar es Salaam.
    Muga amesema kwamba hukumu kwenye shauri hilo namba 20/2018 imetolewa leo na Jaji Wilfred Ndyasobera baada ya kuridhika na hoja zilizotolewa na mawakili wa Wambura, Dk. Masumbuko Lamwai na Emmanuel Muga.
    Maamuzi hayo yanatokana na maombi yaliyowasilishwa Mahakama Kuu wiki mbili zilizopita yakiomba Mahakama imruhusu Wambura afungue kesi ya msingi kuomba kutengua maamuzi ya Kamati za TFF.

    Michael Wambura (kulia) akiwa na mmoja na Mawakili wake, Emmanuel Muga (kushoto)

    Mahakama imetamka kuwa Wambura ana kesi yenye misingi mizito na ambayo inafaa isikilizwe na Mahakama; kwa Kiingereza alisema: ‘Wambura has fit case for further consideration by this court”
    Muga amesema kwamba Mahakama imeridhika kuwa maombi yaliletwa ndani ya muda, na Wambura ana maslahi mapana ya kuleta maombi, hivyo mahakama imempa ruksa ya kuleta kesi ya msingi ya kuomba kutenguliwa kwa maamuzi ya kamati za TFF.
    Amesema Mahakama imeamuru kuwa kesi ya msingi ifunguliwe ndani ya siku 14 kuanzia leo, kwa hiyo kesi hiyo itafunguliwa kama mahakama ilivyoagiza.
    "Maombi ya mapitio yaani Judicial Review ni haki ya msingi inayotafutwa pale chombo kilichotoa maamuzi kilivunja sheria au kukiuka misingi ya haki kama haki ya kusikilizwa,".
    "Tunaamini hii haitachukuliwa kama Wambura amepeleka mpira mahakamani, kwani, hii ni judicial review ya maamuzi ambayo yalivunja sheria za TFF wenyewe, pia hayakufuata misingi ya haki ya kusikilizwa,".
    "Mahakama ipo kwa mujibu wa sheria za nchi, na TFF inafuata sheria hizo, ndio maana wamesajiliwa kwa sheria za BMT, na pia waliapishwa na msajili wa vyama vya michezo kwa mjibu wa sheria hiyo," amesema Muga.
    Machi 15, mwaka huu Kamati ya Maadili ya TFF ilimfungia maisha Wambura kutojihusisha na masuala ya soka kwa makosa matatu, ikisema hatua hiyo imechukuliwa kwa mujibu wa kifungu cha 73(1) (c) cha Kanuni za Maadili ya TFF Toleo la 2013. 
    Hiyo ni baada ya kikao chake cha Machi 14, ambacho pamoja na mambo mengine, kilimjadili Wambura aliyefikishwa kwenye kamati hiyo kwa makosa matatu ya kupokea fedha za TFF malipo yasiyo halali, kugushi  barua na kushusha hadhi ya TFF.
    Wambura alifikishwa kwenye kamati ya Maadili na Sekretarieti ya TFF baada ya Kamati ya Ukaguzi kukutana na kupitia mambo mbalimbali ya ukaguzi na suala hilo la Wambura kuonekana linatakiwa kufika kwenye Kamati ya Maadili.
    Lakini baadaye Wambura alipinga uamuzi huo, akisema Kamati iliyomfungia haina mamlaka, kwa sababu yeye anawajibika kwenye Kamati ya Utendaji na Mkutano Mkuu na akasema atachukua kudai haki yake. 
    Baada ya kimya cha muda wote huo, leo Wambura anaibukia kwenye Mahakama Kuu akitimiza kile alichosema kuchukua hatua katika kudai haki yake.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MAHAKAMA KUU YAMKUBALIA WAMBURA KUZIFUNGULIA KESI KAMATI ZA TFF Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top