• HABARI MPYA

    Saturday, May 19, 2018

    AZAM FC YAPANIA KUIADHIBU TANZANIA PRISONS KESHO CHAMAZI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    TIMU ya Azam FC imedhamiria kuifunga Tanzania Prisons katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kesho Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
    Timu hizo zinatarajia kuumana Jumapili hii katika Uwanja wa Azam Complex kuanzia Saa 2:00 usiku, ukiwa ni mchezo wa raundi ya 29 ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).
    Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB, Maji safi ya Uhai Drinking Water na Tradegents, tayari imeanza kunoa makali kuelekea mchezo huo huku kikosi hicho kikiwa kimeingia kambini jana jioni.
    Kocha Msaidizi wa Azam FC, Idd Nassor Cheche, amesema kwamba kikosi hicho kimeanza vema maandalizi yake huku akikiri ushindani mkubwa unaoonyeshwa na wachezaji mazoezini.

    “Kila mtu anaonyesha ari ya kutaka kucheza kwa hiyo tutarajie tutakuwa na mechi ya ushindani na mechi ya burudani vilevile,” alisema.
    Akizungumzia utofauti wa mchezo huo ukilinganisha na ule wa kwanza waliocheza Uwanja wa Sokoine na kuichapa Prisons mabao 2-0, Cheche alidai kuwa; “Mchezo wa kwanza ushapita na huo unaokuja ni mwingine tofauti na ule wa mwanzo.
    “Kwa hiyo tunajipanga tofauti na vile tulivyojipanga mwanzo kwa sababu mwanzoni tulicheza uwanja tofauti na tulikuwa na baadhi ya wachezaji ambao sasa hivi hawapo, lakini sasa hivi tunajipanga kivingine kuhakikisha tunaendeleza ubabe wetu.”
    Mabao ya Azam FC kwenye mchezo huo wa ugenini, yalifungwa na washambuliaji Yahya Zayed na Paul Peter.
    Alisema kuwa kwa sasa haifikirii mechi ya mwisho dhidi Yanga, anachoangalia ni mchezo ujao dhidi ya Prisons kuhakikisha wanaendeleza ubabe kabla ya kujipanga tena kukipiga na Wanajangwani hao.
    Matajiri hao kutoka viunga vya Azam Complex, wataingia kwenye mchezo huo wakitoka kuifunga Majimaji 2-0, matokeo yaliyoifanya kuzidi kujikita katika nafasi ya pili kwa pointi 52, ikiizidi Yanga kwa pointi nne ambayo ina mechi mbili mkononi huku tayari Simba ikiwa imeshatangaza ubingwa na pointi zake 68.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM FC YAPANIA KUIADHIBU TANZANIA PRISONS KESHO CHAMAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top