• HABARI MPYA

  Saturday, June 01, 2019

  NI AZAM FC MABINGWA AZAM SPORTS FEDERATION CUP, WAIPIGA LIPULI FC 1-0 ILULU

  Na Issa Omar, LINDI
  TIMU ya Azam FC imefanikiwa kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Lipuli FC ya Iringa jioni ya leo Uwanja wa Ilulu mjini Lindi.
  Pongezi kwa mfungaji wa bao hilo pekee kwenye mchezo huo, mshambuliaji Mzambia, Obrey Chirwa aliyefunga bao hilo dakika ya 64 baada ya kumzidi nguvu, beki wa Lipuli FC Ramadhani Haruna Shamte na kumuacha chini, kabla ya kufumua shuti lililomshinda kipa Mohammed Yussuf.
  Kwa ushindi huo, Azam FC inarejea kwenye michuano ya Afrika na itashiriki Kombe la Shirikisho, huku mabingwa wa Ligi Kuu, Simba SC wakicheza Ligi ya Mabingwa.

  Mshambuliaji Mzambia, Obrey Chirwa (kushoto) akishangilia na beki Mghana, Daniel Amoah baada ya kufunga bao pekee leo

   
  Azam FC wanakuwa mabingwa wa nne wa michuano hiyo tangu irejeshwe mwaka 2016, baada ya Yanga SC, Simba SC mwaka 2017 na Mtibwa Sugar mwaka 2018.
  Mwaka 2016 Fainali ilifanyika Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, 2017 Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma na 2018 mambo yalikuwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha.   
  Kwa Azam FC hilo linakuwa taji la tatu msimu huu, baada ya awali kutwaa Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame na baadaye Kombe la Mapinduzi, ikiwa chini ya kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm aliyeondolewa mapema mwaka huu baada ya timu kupoteza mwelekeo.
  Azam FC imeshinda taji la Azam Sports Federation Cup ikiwa chini ya makocha wa muda, Meja Mstaafu Abdul Mingange na Iddi Nassor ‘Cheche’, walimu wa timu za vijana waliopewa kikosi cha kwanza baada ya kufukuzwa kwa Pluijm na Juma Mwambusi aliyekuwa Msaidizi wake.  
  Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa aliwakabidhi Kombe mabingwa wapya wa ASFC baada ya mchezo katika Uwanja uliopendezeshwa kwa mapambo ya wadhamini, Azam TV.
  Beki wa zamani wa Simba SC, Paul Ngalema wa Lipuli FC alichaguliwa Mchezaji Bora wa Mechi, kiungo mshambuliaji wa zamani wa Azam FC, Seif Abdallah Karihe akapewa tuzo ya Ufungaji Bora na beki wa klabu hiyo, Aggrey Morris akapewa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mashindano.
  Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Razack Abalora, Nico Wadada, Daniel Amoah, Yakubu Mohamed, Aggrey Morris, Salmin Hoza, Mudathir Yahya/Frank Domayo dk62, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Obrey Chirwa, Donald Ngoma/Daniel Lyanga dk90 na Bruce Kangwa.
  Lipuli FC; Mohammed Yussuf, William Lucian ‘Gallas’, Paul Ngalema, Novaty Lufunga, Haruna Shamte, Freddy Tangalu, Miraj Athumani, Jimmy Mwaisondola, Paul Nonga, Daruwesh Saliboko/Steven Mganda dk70 na Zawadi Mauya/Seif Karihe dk87.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NI AZAM FC MABINGWA AZAM SPORTS FEDERATION CUP, WAIPIGA LIPULI FC 1-0 ILULU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top