• HABARI MPYA

  Tuesday, June 11, 2019

  BENCHI LA UFUNDI TAIFA STARS LAONGEZEWA MAKOCHA WAWILI WOTE RAIA WA MISRI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  BENCHI la Ufundi la timu ya taifa ya soka ya Tanzania, Taifa Stars limeongezewa nguvu kambini mjini Alexandria kuelekea Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) zikazofanyika baadaye mwezi huu nchini Misri. 
  Hiyo ni baada ya kuongezwa kwa makocha wawili wasaidizi wote raia wa Misri, Abelrahman Essa anayeshughulika na mazoezi ya utimamu wa mwili na Ali Taha ambaye ni Mtathmini mchezo aliyebobea.
  Wawili hao tayari wapo kambini mjini Alexandria na wanaungana na Kocha Mkuu Emmanuel Amunike na Kocha Msaidizi Hemed Suleiman ‘Morocco’ kukamilisha benchi madhubuti la wataalamu wanne Taifa Stars.
  Taifa Stars itaanza na mchezo wa kirafiki dhidi ya wenyeji wa AFCON, Misri Juni 13, mwaka huu Uwanja wa Borg El Arab mjini Alexandria.

  Nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta akiwa mazoezini na wenzake leo mjini Alexandria

  Baada ya hapo Taifa Stars itacheza mechi zake tatu za Kundi C mfululizo ikianza na Senegal Juni 23, Kenya Juni 27 na kumaliza na Algeria Julai 1 kuangalia matokeo yake kama yataipeleka hatua ya mtoano.  
  Mbali na Taifa Stars kupangwa Kundi C AFCON 2019 pamoja na jirani zao, Kenya, Algeria na Senegal – wenyeji, Misri wapo Kundi A pamoja na na Zimbabwe, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
  Kundi B linaundwa na Burundi, Madagascar, Guinea na Nigeria, Kundi D linaundwa na Namibia, Afrika Kusini, Ivory Coast na Morocco, wakati Kundi E kuna Angola, Mauritania, Mali na Tunisia na Kundi F ni Guinea Bessau, Benin, Ghana na mabingwa watetezi, Cameroon. 
  Michuano itaanza Juni 21 hadi Julai 19 na Taifa Stars itachezea mechi zake Uwanja wa Juni 30 na Al Salam mjini Cairo.
  Na katika CHAN, Taifa Stars itaanzia nyumbani dhidi ya Sudan Julai 26 kabla ya kurudiana Agosti 2 na ikifuzu mtihani huo itamenyana na mshindi kati ya Kenya na Burundi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: BENCHI LA UFUNDI TAIFA STARS LAONGEZEWA MAKOCHA WAWILI WOTE RAIA WA MISRI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top