• HABARI MPYA

  Friday, June 28, 2019

  YANGA SC KUANIKA KIKOSI KIPYA JULAI 27 TAIFA KWA MCHEZO WA KIRAFIKI WA KIMATAIFA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  YANGA SC itacheza mechi ya kwanza ya msimu Julai 27 mwaka huu Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam dhidi ya wapinzani kutoka nje ya nchi.
  Hayo yamesemwa mchana wa leo na Mwenyekiti wa Yanga SC, Dk. Mshindo Msolla katika mkutano na Waandishi wa Habari makao makuu ya klabu, makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani mjini Dar es Salaam. 
  “Tarehe 27/07 tutakuwa na matukio matatu, moja ni kutambulisha jezi, pili kutambulisha wachezaji wapya na tatu ni tutakuwa na mchezo kimataifa wa kirafiki,”amesema Dk. Msolla, kocha wa zamani wa Taifa Stars. 
  Aidha, Dk. Msolla amesema kwamba usajili walioufanya ni mzuri kwa sababu umezingatia vigezo vya kitaalamu kimpira. 

  Mwenyekiti wa Yanga SC, Dk. Mshindo Msolla (kulia) akizungumza na Waandishi wa Habari leo makao makuu ya klabu 

  “Tumesajili kulingana na matakwa ya mwalimu, hata huko alipo lazima atakuwa ana furaha, maana wachezaji wote wa nje na ndani aliokuwa akiwahitaji tumewapata, pia siku tatu zilizopita mwalimu alituma programu ya mazoezi, sisi kama menejimenti tumejipanga kuhakikisha yote yanaenda sawa,”amesema Dk. Msolla.
  Hadi sasa Yanga SC tayari imekwishasajili wachezaji wapya 10, ambao ni beki Ally Ally kutoka KMC ya Kinondoni, viungo wa ulinzi, Abdulaziz Makame kutoka Mafunzo ya Zanzibar, Mapinduzi Balama kutoka Alliance FC ya Mwanza, Sadney Urikhob kutoka Namibia, Lamine Moro kutoka Ghana, Juma Balinya kutoka Uganda, Issa Bigirimana, Patrick Sibomana wote wa Rwanda, Mustapha Seleman kutoka Burundi na Maybin Kalengo kutoka Zambia.
  Kwa upande mwingine, Dk. Msolla amewapa siku nne wote wanaotumia nembo ya klabu kwa ajili ya utengenezaji wa jezi na vifaa mbalimbali kuacha mara moja.
  Dk. Msolla amesema kwamba baada ya Juni 30 mtu yeyote atakayejihusisha na uuzaji wa jezi feki hatua kali za kisheria zitachukuliwa juu yake.
  Mwenyekiti amesema kwamba lengo la kuwaita watu hao wanaojihusisha na uuzaji wa jezi ni kufanya nao mazungumzo ni kujua ni namna gani wanaweza kusaidiana kwenye suala hilo la mauzo ya jezi na vifaa mbalimbali vyenye nembo ya klabu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA SC KUANIKA KIKOSI KIPYA JULAI 27 TAIFA KWA MCHEZO WA KIRAFIKI WA KIMATAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top