• HABARI MPYA

  Tuesday, June 11, 2019

  MWADINI AFICHUA SIRI YA MAFANIKIO YAKE HADI AMEDUMU AZAM FC

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KIPA mkongwe wa Azam FC, Mwadini Ali amesema kwamba siri ya mafanikio yake ni kujitunza na kuzingatia nidhamu ya mazoezi.
  Akizungumza baada ya kusaini mkataba mpya wa mwaka mmoja kuendelea kuitumikia timu ya Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake, Mwadini amesema nidhamu, uadilifu na kujitunza ndiyo siri ya mafanikio yake. 
  "Mimi sina mambo mengi, hata vijana wanajua. Ninajitunza na ninazingatia miiko ya michezo, ni hayo mambo yanayonifanya niwe vizuri siku zote,"amesema Mwadini, ambaye kwa sasa ni kipa wa pili nyuma ya Mghana, Razack Abalora.
  Mwadini Ali amesema kwamba siri ya mafanikio yake ni kujitunza na kuzingatia nidhamu ya mazoezi

  Mwadini alijiunga na Azam FC mwaka 2011 akitokea Mafunzo ya Zanzibar, alisaini mkataba huo rasmi mwishoni mwa wiki mbele ya Ofisa Mtendaji Mkuu, Abdulkarim Amin 'Popat' na Mratibu wa timu, Phillip Alando.
  Mchezaji huyo mwandamizi wa timu hiyo, anazidi kuongeza idadi ya wachezaji waliosaini mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia Azam FC, wengine wakiwa ni mabeki David Mwantika, Bruce Kangwa, Abdallah Kheri na mshambuliaji Donald Ngoma.
  Uongozi wa Azam FC chini ya Popat kwa kushirikiana na benchi la ufundi la timu hiyo, wanaendelea na zoezi la kuwabakisha wachezaji waliomaliza mkataba pamoja na usajili wa wachezaji wapya wa kuongeza nguvu kikosini kwa ajili ya msimu ujao.
  Kikosi cha Azam FC kwa sasa kipo mapumzikoni na kinatarajia kurejea mazoezini Juni 20 mwaka huu, tayari kuanza maandalizi ya msimu mpya 2019/2020 ikianza na kibarua cha kutetea Kombe la Kagame (CECAFA Kagame Cup) kuanzia Julai 6 mwaka huu jijini Kigali, Rwanda.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MWADINI AFICHUA SIRI YA MAFANIKIO YAKE HADI AMEDUMU AZAM FC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top