• HABARI MPYA

  Tuesday, June 11, 2019

  SIMBA SC YASEMA POLOKWANE CITY ILIKIUKA TARATIBU ZA FIFA KATIKA KUMSAJILI BOCCO

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KLABU ya Simba SC imedai Polokwane ya Afrika Kusini ilikiuka utaratibu kumsainisha mkataba mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, John Raphael Bocco ‘Adebayor’.
  Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Simba SC, Hajji Sunday Manara amewaambia Waandishi wa Habari leo kwamba – pamoja na hayo wamefanya mawasiliano na Polokwane na kutatua suala la mchezaji huyo.
  Nahodha huyo wa Simba SC jana ameripotiwa kusaini mkataba mpya wa miaka miwili kuendelea kuichezea klabu hiyo baada ya kufunga mabao 30 katika misimu miwili ya kuwa na Wekundu wa Msimbazi baada ya kuachwa Azam FC.
  Nahodha John Bocco akiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Simba SC, Mohamed 'Mo' Dewji baada ya kusaini mkataba mpya 

  Kipa Aishi Manula akiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Simba SC, Mohamed 'Mo' Dewji baada ya kusaini mkataba mpya

  Lakini inadaiwa kabla ya kusaini mkataba huo alikuwa tayari amesaini mkataba wa kujiunga na Polokwane City FC yenye maskani yake Polokwane, Limpopo inayofundishwa na kocha Mslovakia, Jozef Vukusic.
  Hata hivyo, katika taarifa yake ya leo, Manara amesema kwamba suala hilo lilizungumzwa baina ya uongozi wa Simba SC na Polokwane City FC na wakafikia makubaliano kwamba Bocco ataendelea kuitumikia klabu yake ya sasa.
  “Ifahamike kuwa kwa mujibu wa FIFA (Shirikisho la Soka la Kimataifa), mchezaji akiwa amebakiza miezi sita kabla ya mkataba wake kumalizika, na kama kuna klabu nyingine inayotaka kumsajili inabidi iwape taarifa klabu husika inayommiliki kabla ya kuzungumza na mchezaji,” imesema taarifa ya SImba na kuongeza;
  “Kwenye suala hili la Bocco, Polokwane hawakutoa taarifa kwa Simba SC juu ya kutaka kufanya mazungumzo na Nahodha wetu. Kwa muktadha huo, tunawajulisha wana Simba na Watanzania wote kwa ujumla kwamba John Bocco bado ni mchezaji halali wa Simba SC na amekwishaongeza mkataba na klabu kama tulivyowaarifu jana,”.  
  Pamoja na Bocco, wachezaji wengine wote waliosajiliwa na Simba SC mwaka juzi kutoka Azam FC, kipa Aishi Manula na mabeki wanaoweza kucheza nafasi za kiungo pia, Shomari Kapombe na Erasto Nyoni nao pia wamesaini mikataba mipya baada ya misimu miwili mizuri ya awali.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA SC YASEMA POLOKWANE CITY ILIKIUKA TARATIBU ZA FIFA KATIKA KUMSAJILI BOCCO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top