• HABARI MPYA

  Sunday, June 30, 2019

  SINGIDA UNTED YAANZA KAZI, YASAJILI MSHAMBULIAJI WA GHANA NA BEKI MZANZIBARI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KUFUATIA kufunguliwa rasmi leo kwa dirisha la usajili la Ligi Kuu ya Tanzania Bara, klabu ya Singida United imetaja wachezaji wawili wapya iliyoanza nao katika kujenga kikosi cha msimu mpya.
  Hao ni beki wa kushoto, Muharami Salum ‘Marcelo’ kutoka klabu ya Malindi ya Zanzibar na mshambuliaji Herman Frimpong  kutoka Ghana.
  “Marcelo aliyetikisa Ligi Kuu visiwani Zanzibar na hasa wakati wa Mapinduzi Cup, amejiunga nasi kwa kandarasi ya miaka mitatu. Herman Frimpong ni Ingizo Jipya katika kuimarisha safu ya Ushambuliaji. Huyu ni Raia wa Ghana ambaye amshawasili nchini tayari kwa kuanza pre-season,”imesema taarifa ya Singida United leo.

  Mshambuliaji Herman Frimpong amesaini mkataba wa kujiunga na Singida United kutoka Ghana.

  Taarifa hiyo inakuja muda mfupi baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kufungua dirisha la usajili kwa Klabu za Ligi Kuu, Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la Pili kwa msimu wa 2019/2020.
  Taarifa ya Afisa Habari na Mawasiliano wa TFF, Cliford Mario Ndimbo leo imesema kwamba dirisha litafungwa Julai 31, mwaka huu na hakutakua na muda wa ziada baada ya zoezi hilo kufungwa.
  Taarifa hiyo imesema kwamba ssajili wa mashindano ya CAF kwa Klabu za Simba, Yanga SC, Azam FC na KMC wenyewe utafungwa Julai 10, mwaka huu.
  Baada ya kipindi hicho cha usajili klabu zitakuwa na siku tisa za kusajili kwa kulipa faini ya dola za Kimarekani 250 kuanzia Julai 11 hadi Julai 20, mwaka huu.
  Taarifa imesema kutakuwa na kipindi cha pili cha usajili wa CAF kitakachokua na siku 10 kuanzia Julai 21 hadi Julai 31, 2019 kipindi ambacho watalipa dola 500 na mchezaji ataanza kutumika kuanzia raundi ya pili.
  Simba na Yanga SC wanawakilisha nchi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, wakati Azam FC na KMC wanawakilisha nchi kwenye Kombe la Shirikisho na TFF imesisitiza Klabu zote kufanya usajili kwa wakati.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SINGIDA UNTED YAANZA KAZI, YASAJILI MSHAMBULIAJI WA GHANA NA BEKI MZANZIBARI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top