• HABARI MPYA

  Thursday, June 20, 2019

  ROSTAM AZIZ APINGA YANGA SC KUMILIKIWA NA MTU BINAFSI AU KUWA NA MFADHILI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MFANYABIASHARA maarufu, Rostam Aziz, amesema kwa maoni yake Yanga inastahili kuendelea kuendeshwa kwa michango ya wanachama wake pamoja na vyanzo vingine vya mapato badala ya kumilikiwa na mtu binafsi au kuwa na mfadhili.
  Ametaja vyanzo vingine vya mapato mbali na michango ya wanachama kuwa ni pamoja na wadhamini, makampuni kutangaza bidhaa zao, viingilio vya milangoni, biashara ya bidhaa mbalimbali kwa chapa ya Yanga kama vile jezi pamoja na haki za matangazo ya televisheni.
  Mfanyabiashara huyo ambaye alikuwa akitajwa kuwa na mpango wa kuwekeza katika klabu hiyo amesema kwa mtazamo wake timu kubwa kama Yanga kuwa na mfadhili ni kuziba nafasi kwa wadhamini wengine ambao wangependa kutangaza bidhaa na huduma zao kupitia klabu hiyo, jambo ambalo litaipunguzia mapato.


  “Ufadhili ni mlango wa nyuma wa kumiliki,” amesisitiza Rostam Aziz, Mbunge wa zamani wa jimbo la Igunga na aliyewahi kuwa Mweka Hazina wa Chama cha Mapinduzi (CCM).
  Juni 5, mwaka huu Rostam Aziz alitoa kiasi cha Sh. Milioni 200 kuichangia Yanga SC ifanikishe zoezi la usajili wa kuunda kikosi imara cha msimu ujao.
  Ofa hiyo ya Rostam, Mbunge wa zamani wa Igunga, Tabora na aliyekuwa kuwa Mweka Hazina wa CCM ilitangazwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa katika tamasha la Kubwa Kuliko lilifanyika ukumbi wa Diamond Jubilee mjini Dar es Salaam.
  Pamoja na Rostazm, mfanyabiashara mwingine Ghalib kupitia kampuni yake ya GSM alichangia klabu hiyo Sh. Milioni 300 na kwa ujumla kiasi cha Sh. Bilioni 1 kilipatikana.
  Waziri Mkuu, Majaliwa aliyekuwa mgeni rasmi katika Kubwa Kuliko iliyotikisa mji Jumamosi iliyopita kwa upande wake alitoa Sh. Milioni 10, huku Rais mstaafu wa awamu ya Nne, Jakaya Mrisho Kikwete aliyehudhuria pia shughuli hiyo akitoa kiasi cha Sh. Milkioni 5.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: ROSTAM AZIZ APINGA YANGA SC KUMILIKIWA NA MTU BINAFSI AU KUWA NA MFADHILI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top