• HABARI MPYA

  Monday, June 17, 2019

  TAIFA STARS YATOA SARE 1-1 NA ZIMBABWE MECHI YA KIRAFIKI MISRI

  Na Mwandishi Wetu, CAIRO
  TIMU ya soka ya taifa ya Tanzania imelazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Zimbabwe katika mchezo wa kirafiki Uwanja wa El Sekka El Hadid mjini Cairo. 
  Pongezi kwa Nahodha, Mbwana Ally Samatta anayechezea KRC Genk ya Ubelgiji aliyetokea benchi jana na kuisawazishia Taifa Stars kufuatia Zimbabwe kutangulia.
  Huo ulikuwa mchezo wa pili kwa Taifa Stars wa kujipima nguvu katika kambi yake nchini Misri kujiandaa na Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) baadaye mwezi nchini humo, kufuatia kufungwa 1-0 na wenyeji wa michuano hyo, Mafarao Alhamisi, bao pekee la kiungo wa Aston Villa ya England, Ahmed El Mohamady.
  Mshambuliaji wa Tanzania, Thomas Ulimwengu akitafuta maarifa ya kumpita mchezaji wa Zimbabwe
  Taifa Stars itacheza mechi zake tatu za Kundi C AFCON 2019 mfululizo dhidi ya Senegal Juni 23, Kenya Juni 27 na Algeria Julai 1 kisha kuangalia matokeo yake kama yataipeleka hatua ya mtoano.  
  Mbali na Taifa Stars kupangwa Kundi C AFCON 2019 pamoja na jirani zao, Kenya, Algeria na Senegal – Zimbabwe wapo Kundi A pamoja na wenyeji, Misri, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
  Kundi B linaundwa na Burundi, Madagascar, Guinea na Nigeria, Kundi D linaundwa na Namibia, Afrika Kusini, Ivory Coast na Morocco, wakati Kundi E kuna Angola, Mauritania, Mali na Tunisia na Kundi F ni Guinea Bessau, Benin, Ghana na mabingwa watetezi, Cameroon. 
  Taifa Stars imefuzu AFCON ya mwaka huu baada ya kumaliza nafasi ya pili kwenye Kundi L kwa pointi zake nane, nyuma ya jirani zao wa Afrika Mashariki, Uganda walioongoza kwa pointi zao 13 wakizipiku Lesotho iliyomaliza na pointi sita na Cape Verde pointi tano.    
  Mwaka huu, Tanzania itashiriki AFCON kwa mara ya pili tu kihistoria baada ya mwaka 1980 nchini Nigeria ambako ilipangwa Kundi A pamoja na wenyeji, Nigeria, Misri na Ivory Coast na kushika mkia.
  Mwaka 1980 ilifungwa mechi mbili, 3-1 na Nigeria na 2-1 na Misri kabla ya kutoa sare ya 1-1 na Ivory Coast na kuishia Raundi ya kwanza tu, wakati timu nane tu zinashiriki michuano hiyo.   
  Michuano itaanza Juni 21 hadi Julai 19 na Taifa Stars itachezea mechi zake Uwanja wa Juni 30 na Al Salam mjini Cairo.
  Na katika CHAN, Taifa Stars itaanzia nyumbani dhidi ya Sudan Julai 26 kabla ya kurudiana Agosti 2 na ikifuzu mtihani huo itamenyana na mshindi kati ya Kenya na Burundi.
  Kikosi cha Tanzania kilikuwa; Metacha Mnata/Aaron Kalambo, Vincent Philipo, Gardiel Michael, Ally Sonso, Erasto Nyoni/Kelvin Yondan, Frank Domayo/Feisal Salum, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Yahya Zayd/Farid Mussa, Adi Yussuf/Simon Msuva, Thomas Ulimwengu na Rashid Mandawa/Mbwana Samatta.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TAIFA STARS YATOA SARE 1-1 NA ZIMBABWE MECHI YA KIRAFIKI MISRI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top