• HABARI MPYA

  Friday, June 14, 2019

  TAIFA STARS YACHAPWA 1-0 NA MISRI SALAH NA EL NENY WAKIWA BENCHI ALEXANDRIA

  Na Mwandishi Wetu, ALEXANDRIA
  TIMU ya soka ya taifa ya Tanzania imechapwa bao 1-0 na wenyeji, Misri katika mchezo wa kirafiki leo Uwanja wa Borg El Arab mjini Alexandria.
  Bao pekee la wenyeji kwenye mchezo huo maalum kujiandaa na Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) zinazotarajiwa kuanza Juni 21 hadi Julai 19 nchini Misri limefungwa na kiungo wa Aston Villa ya England, Ahmed El Mohamady dakika ya 64 akimalizia pasi ya beki wa Pyramids ya nyumbani, Ahmed Ayman Mansour.
  Pamoja na kufungwa, Taifa Stars inayofundishwa na Mnigeria, Emmanuel Amunike ikiongozwa na Nahodha wake, mshambuliaji wa KRC Genk ya Ubelgiji, Mbwana Samatta ilicheza vizuri – lakini ukweli tu ilizidiwa na Mafarao.
  Nahodha wa Tanzania, Mbwana Samatta akimtoka beki wa Misri, Mahmoud Alaa leo  
  Mbwana Samatta (wa pili kulia) katika picha ya pamoja na marefa na Nahodha na mfungaji wa bao la Misri leo, Ahmed El Mohamady (wa pili kushoto) kabla ya mchezo wa leo 

  Kocha Mmexico anayeinoa Misri aliwaacha benchi muda wote wa mchezo nyota wa Ligi Kuu ya England, kiungo Mohamed Elneny wa Arsenal na mshambuliaji Mohamed Salah wa Liverpool.
  Taifa Stars itacheza mechi zake tatu za Kundi C AFCON 2019 mfululizo dhidi ya Senegal Juni 23, Kenya Juni 27 na Algeria Julai 1 kisha kuangalia matokeo yake kama yataipeleka hatua ya mtoano.  
  Mbali na Taifa Stars kupangwa Kundi C AFCON 2019 pamoja na jirani zao, Kenya, Algeria na Senegal – wenyeji, Misri wapo Kundi A pamoja na na Zimbabwe, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
  Kundi B linaundwa na Burundi, Madagascar, Guinea na Nigeria, Kundi D linaundwa na Namibia, Afrika Kusini, Ivory Coast na Morocco, wakati Kundi E kuna Angola, Mauritania, Mali na Tunisia na Kundi F ni Guinea Bessau, Benin, Ghana na mabingwa watetezi, Cameroon. 
  Taifa Stars imefuzu AFCON ya mwaka huu baada ya kumaliza nafasi ya pili kwenye Kundi L kwa pointi zake nane, nyuma ya jirani zao wa Afrika Mashariki, Uganda walioongoza kwa pointi zao 13 wakizipiku Lesotho iliyomaliza na pointi sita na Cape Verde pointi tano.    
  Mwaka huu, Tanzania itashiriki AFCON kwa mara ya pili tu kihistoria baada ya mwaka 1980 nchini Nigeria ambako ilipangwa Kundi A pamoja na wenyeji, Nigeria, Misri na Ivory Coast na kushika mkia.
  Mwaka 1980 ilifungwa mechi mbili, 3-1 na Nigeria na 2-1 na Misri kabla ya kutoa sare ya 1-1 na Ivory Coast na kuishia Raundi ya kwanza tu, wakati timu nane tu zinashiriki michuano hiyo.   
  Michuano itaanza Juni 21 hadi Julai 19 na Taifa Stars itachezea mechi zake Uwanja wa Juni 30 na Al Salam mjini Cairo.
  Na katika CHAN, Taifa Stars itaanzia nyumbani dhidi ya Sudan Julai 26 kabla ya kurudiana Agosti 2 na ikifuzu mtihani huo itamenyana na mshindi kati ya Kenya na Burundi.
  Kikosi cha Misri kilikuwa; Ahmed Al Shenawy/Mahmoud Gennesh dk46, Ahmed Hegazi, Ayman Ashraf/Ahmed Ayman Mansour dk46, Mahmoud Alaa, Ahmed El Mohamady, Abdalla El Said, Walid Soliman/Mahmoud Ibrahim Hassan ‘Trezeguet’ dk61, Tarek Hamed/Ali Ghazal, Amr Warda/Marwan Mohsen dk89, Nabil Emad Dunga na Ahmed Ali/Ahmed Hassan Mahgoub ‘Koka’ dk46.  
  Tanzania; Aishi Manula, Gardiel Michael, Hassan Kessy, Aggrey Morris/Ally Sonso dk74, Kelvin Yondani, Himid Mao, Simon Msuva, Feisal Salum, John Bocco/Thomas Ulimwengu dk62, Mbwana Samatta na Farid Mussa/Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ dk78.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TAIFA STARS YACHAPWA 1-0 NA MISRI SALAH NA EL NENY WAKIWA BENCHI ALEXANDRIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top