• HABARI MPYA

  Thursday, June 20, 2019

  SIMBA SC YAMSAJILI KIUNGO BORA WA LIGI KUU YA SUDAN MARA MBILI MFULULIZO

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KIUNGO wa kimataifa wa Sudan, Sharaf Eldin Shiboub Ali Abdalrahman amesaini mkataba wa mwaka mmoja kujiunga na mabingwa wa Tanzania, Simba SC.
  Sharaf Abdalrahman anatua Mtaa wa Msimbazi akitokea klabu ya Al Hilal ya nyumbani kwao ambayo ameitumikia kwa mafanikio makubwa.
  Mchezaji huyo ametambulishwa rasmi leo mchana kwa picha zilizopostiwa kwenye ukurasa rasmi wa Instagram wa Simba SC akiwa mmoja wa Wakurugenzi wa klabu hiyo, Salum Abdallah ‘Try Again’.

  Mmoja wa Wakurugenzi wa Simba SC, Salum Abdallah 'Try Again' akimtambulisha mchezaji mpya, Sharaf Eldin Shiboub Ali Abdalrahman baada ya kusaini mkataba wa mwaka mmoja  
   Sharaf Eldin Shiboub Ali Abdalrahman akisaini mkataba wa mwaka mmoja kujiunga na Simba
  Wakala wa Eldin Shiboub Ali Abdalrahman baada ya kumalizana na Simba

  “Kiungo bora mara mbili mfululizo wa Ligi Kuu ya Sudan na mchezaji wa timu ya Taifa ya Sudan tangu akiwa na miaka 17 akitokea kwa mabingwa mara tatu mfululizo wa Ligi Kuu ya Sudan klabu ya Al Hilal, Sharaf Eldin Shiboub Ali Abdalrahman amejiunga na Mabingwa wa nchi kwa mkataba wa mwaka mmoja. Karibu Msimbazi Sharaf,”imesema taarifa ya SImba leo.
  Sharaf Abdalrahman anakuwa mchezaji mpya wa tatu tu rasmi kusajiliwa na Simba SC, baada ya kipa Beno Kakolanya kutoka Yanga SC na beki wa kati, Kennedy Wilson Juma kutoka Singida United wote Watanzania.
  Lakini tayari kuna taarifa za klabu kuwa kwenye mazungumzo na mawakala wa wachezaji kadhaa na wengine imeripotiwa wapo njiani nchini.
  Miongoni mwao ni beki wa kati Mbrazil, Gerson Fraga Vieira kutoka ATK ya India na mshambuliaji Ryan Moon kutoka Kaizer Chiefs ya kwao, Afrika Kusini.
  Wakati huo huo: Kikosi cha Simba SC kimeondoka Dar es Salaam leo asubuhi kwa ndege kwenda Misungwi kupitia Mwanza mjini kwa ajili ya mchezo wa kirafiki dhidi ya wenyeji, Gwambina FC.
  Huo utakuwa mchezo maalum wa ufunguzi wa Uwanja wa klabu ya Gwambina inayoshiriki Ligi Daraja la Pili Tanzania Bara.
  Miongoni mwa wachezaji waliokwenda huko ni pamoja na beki mpya, Kennedy Wilson Juma, Yusufu Mlipili, Hassan Dilunga, Said Ndemla na wengineo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA SC YAMSAJILI KIUNGO BORA WA LIGI KUU YA SUDAN MARA MBILI MFULULIZO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top