• HABARI MPYA

  Tuesday, June 11, 2019

  MEDDIE KAGERE APANIA KUENDELEA KUFANYA VIZURI KATIKA LIGI KUU YA TANZANIA BARA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Rwanda, Meddie Kagere amesema kwamba ataendelea kung’ara kwenye Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu ujao, kwa sababu anaamini juu ya uwezo wake.
  Akizungumza baada ya kutajwa mshindi wa tuzo ya Mchezaji Bora wa mwisho wa mwezi wa Ligi Kuu, mchezaji huyo wa Simba SC amesema kwamba nia yake ni kuendelea kufanya vizuri.
  “Ninamshukuru Mungu kwa mafanikio haya, na nia yangu ni kuendelea kufanya vizuri na msimu ujao pia nikiwa na klabu yangu (Simba),”amesema Kagere aliyejiunga na Simba SC msimu huu kutika Gor Mahia ya Kenya.
  Meddie Kagere amesema ataendelea kung’ara kwenye Ligi Kuu ya Bara msimu ujao 
      
  Kagere alifunga ukurasa wa wachezaji bora wa mwezi wa Ligi Kuu msimu wa 2018/2019, baada ya kuwashinda Mrundi Bigirimana Blaise wa Alliance FC ya Mwanza na Tariq Kiakala wa Biashara United ya Mara alioingia nao fainali katika uchambuzi uliofanywa Dar es Salaam wiki iliyopita na Kamati ya Tuzo ya TPL inayotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
  Kwa mwezi huo wa Mei, Simba ilicheza michezo nane na kushinda minne, sare tatu na kupoteza mija, ambapo Kagere alitoa mchango mkubwa kwa timu yake akifunga mabao sita na kuifanya Simba ipande kutoka nafasi ya pili hadi ya kwanza na kutwaa ubingwa.
  Kwa upande wa Bigirimana yeye aliiongoza Alliance iliyocheza mechi tano ikishinda tatu, sare moja na kupoteza moja, ambapo alifunga mabao mawili na timu yake ilipaa kutoka nafasi ya 17 hadi ya 11 katika msimamo wa ligi. Kiakala yeye aliiwezesha Biashara kushinda mchezo mmoja, sare mbili na kupoteza moja na kuepuka balaa la kushuka daraja.
  Aidha, Kamati ya Tuzo pia imemchagua Kocha Mkuu wa KMC, Etienne Ndayiragije kuwa Kocha Bora wa Mwezi Mei akiwashinda Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems na Kocha Mkuu wa Alliance, Malale Hamsini.
  Ndayiragije aliiongoza KMC katika michezo mitano iliyocheza ikishinda minne na sare moja ikivuna pointi 13 kati ya 15, ikipaa kutoka nafasi ya sita hadi ya nne, wakati Aussems aliiongoza Simba katika michezo nane, ikishinda minne, sare tatu na kupoteza moja ikivuna pointi 15 kati ya 24.
  Kwa upande wa Malale Hamsini aliiongoza Alliance katika michezo mitano ikishinda mitatu, sare moja na kufungwa moja ikivuna pointi 10 kati ya 15 na kupanda kutoka nafasi ya 17 hadi ya 11 katika msimamo wa ligi.
  Washindi watazawadiwa sh. 1,000,000 (milioni moja) kila mmoja, kikombe (trophy) kutoka wadhamini wa tuzo hizo za mwezi Biko Sports pamoja na kisimbusi kutoka Azam TV wenye haki za matangazo ya televisheni ya Ligi Kuu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MEDDIE KAGERE APANIA KUENDELEA KUFANYA VIZURI KATIKA LIGI KUU YA TANZANIA BARA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top