• HABARI MPYA

  Sunday, June 30, 2019

  WINGA MACHACHARI WA TP MAZEMBE, DEO KANDA MUKOKO ATUA SIMBA SC KWA MKOPO

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  WINGA wa kimataifa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Deo Gracia Kanda Mukoko anatarajiwa kujiunga na klabu ya Simba ya Dar es Salaam kwa mkopo kutoka TP Mazembe ya Lubumbashi.
  Taarifa ya TP Mazembe leo imesema kwamba Kanda amekuja Tanzania kukamilisha mipango ya kujiunga na mabingwa wa Tanzania kwa mkopo wa msimu mmoja.
  Hakukuwa na ufafanuzi zaidi juu ya mpango huo, lakini taarifa zisizo rasmi zinasema Simba SC wanapewa Kanda kwa mkopo baada ya kukubali kumuachia kiungo mshambuliaji, Ibrahim Ajibu iliyemsajili tena kutoka kwa mahasimu, Yanga.

  Deo Kanda Mukoko anatarajiwa kujiunga na Simba kwa mkopo kutoka TP Mazembe ya Lubumbashi

  Inadaiwa Simba SC wamerejeshewa fedha zao walizompa Ajibu na kupewa Kanda kwa mkopo baada ya mazungumzo ya kiungwana yaliyozaa makubaliano hayo. 
  Kanda alitua kwa mara ya kwanza Mazembe mwaka 2009 na alikuwemo kwenye kikosi cha timu hiyo kilichoshiriki klabu bingwa ya dunia ya FIFA mwaka 2010, kabla ya kuhamia Raja Casablanca ya Morocco mwaka 2013.
  Alicheza Morocco kwa msimu mmoja kabla ya mwaka 2014 kurejea nyumbani, DRC na kujiunga AS Vita alikocheza kwa msimu mmoja pia kisha akajiunga tena na Mazembe mwaka 2015 hadi sasa anatolewa kwa mkopo.
  Wakati huo huo: Simba SC kesho inatarajiwa kusaini mkataba wa udhamini na kampuni ya A-One, watengenezaji wa kinywaji cha Mo-Extra.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: WINGA MACHACHARI WA TP MAZEMBE, DEO KANDA MUKOKO ATUA SIMBA SC KWA MKOPO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top