• HABARI MPYA

  Friday, June 28, 2019

  TAIFA STARS YAGONGWA 3-2 NA HARAMBEE STARS NA KUTUPWA NJE MICHUANO YA AFCON

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  TANZANIA imetupwa nje ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika baada ya kuchapwa 3-2 na Kenya katika mchezo wa Kundi C usiku huu Uwanja wa Juni 30 mjini Cairo.
  Baada ya kufungwa 2-0 na Senegal kwenye mchezo wa kwanza, sasa Taifa Stars itaingia kwenye mchezo wa mwisho dhidi ya Algeria Julai 1 kukamilisha ratiba na kusaka heshima, wakati Kenya itahitaji ushindi mbele ya Senegal kuangalia uwezekano wa kusonga mbele kufuatia kupoteza mechi ya kwanza.
  Katika mchezo wa leo uliokuwa mkali na wa kusisimua, kiungo mshambuliaji wa Difaa Hassan El-Jadidi ya Morocco, Simon Happygod Msuva alianza kuifungia Taifa Stars bao zuri na la mapema dakika ya sita tu ya mchezo.
  Kipa wa Tanzania, Aishi Manula akiokoa moja ya hatari kwenye mchezo huo 

  Manahodha; Mbwana Samatta wa Tanzania (wa pili kulia) na Victor Wanyama wa Kenya (wa pili kushoto) kabla ya mchezo huo

  Lakini mshambuliaji wa Kashiwa Reysol ya Japan aliyewahi kuchezea Girona ya Hispania kwa mkopo, Michael Ogada Olunga akaisawazishia Harambee Stars kwa tik tak dakika ya 39 akitumia makosa ya kipa wa Simba SC, Aishi Salum Manula kutema mpira. 
  Hata hivyo, bao hilo la mshambuliaji huyo wa zamani wa Tusker, Thika United, Gor Mahia za nyumbani kwao, Kenya zote akicheza kwa mkopo kutroka kademi ya Liberty Sports kabla ya kuuzwa Djurgardens IF ya Sweden ambayo nayo ilimuuza Guizhou Zhicheng ya China halikudumu sana.
  Kwani dakika moja baadaye, Nahodha wa Tanzania na mshambuliaji wa KRC Genk ya Ubelgiji, Mbwana Ally Samatta akaifungia bao la pili Taifa Stars baada ya jitihada binafasi akiwapangua mabeki wa Kenya na kumtungua kwa shuti kali kipa wa Saint George ya Ethiopia, Patrick Musotsi Matasi.
  Kipindi cha pili Harambee Stars walio chini ya kocha Mfaransa, Sebastien Migne walikuwa na moto na kupeleka mashambulizi mfululizo langoni mwa Taifa Stars inayofundishwa na Mnigeria, Emmanuel Amunike.
  Na jitihada zao zaikazaa matunda dakika ya 62 baada ya kiungo wa Cercle Brugge ya Ubelgiji, Johanna Ochieng Omolo kufunga bao la kusawazisha akimalizia kazi nzuri ya mshambuliaji wa Beijing Renhe ya China, Ayub Timbe Masika aliyewahi kucheza Lierse SK ya Ubelgiji.
  Olunga akaifungia Harambee Stars bao la ushindi dakika ya 80 akimalizia kazi nzuri ya mtokea benchi, kiungo wa IF Brommapojkarna ya Sweden, Eric Johana Omondi.
  Kikosi cha Kenya kilikuwa; Patrick Matasi, Musa Mohammed, David Owino/Bernard Oginga dk46, Aboud Khamis/ Eric Omondi dk68, Joseph Okumu, Erick Ouma Otieno, Victor Wanyama, Johanna Omolo, Francis Kahata/John Avire dk33, Ayub Masika na Michael Olunga.
  Tanzania;  Aishi Manula, Gardiel Michael, Hassan Kessy, Kelvin Yondani, David Mwantika, Erasto Nyoni/Frank Domaro dk80, Mudathir Yahya/Himid Mao dk52, Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu/John Bocco dk70, Simon Msuva na Farid Mussa.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TAIFA STARS YAGONGWA 3-2 NA HARAMBEE STARS NA KUTUPWA NJE MICHUANO YA AFCON Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top