• HABARI MPYA

  Saturday, June 01, 2019

  MAKAMBO AWAAGA YANGA SC NA KWENDA KUANZA MAISHA MAPYA HOROYA YA GUINEA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Heritier Ebenezer Makambo ameaga na kuondoka klabu ya Yanga ya Dar es Salaam baada ya kuitumikia kwa mwaka mmoja.
  Makambo anakwenda kujiunga na klabu ya Horoya AC ya Guinea ambako alisaini mkataba wa miaka mitatu wiki mbili zilizopita, ingawa Yanga ilikwepa kuthibitisha moja kwa moja kumruhusu mchezaji huyo.
  Mwenyekiti mpya wa klabu ya Yanga, Dk. Mshindo Msolla alithibitisha kumruhusu Kocha Mkuu wa klabu, Mwinyi Zahera kwenda na Makambo Guinea kwa mazungumzo na Horoya Athletic Club, lakini akasema si kwa kumuuza bali kufuata ofa ya klabu hiyo.

  Heritier Makambo amesaini mkataba wa miaka mitatu kujiunga na Horoya AC ya Guinea 

  Lakini Makambo mwenyewe aliporejea akaweka wazi kwamba amekwishamalizana na klabu hiyo na baada ya msimu atakwenda Guinea kuanza maisha mapya.
  Na japokuwa Makambo ameaga na kuondoka, lakini bado uongozi wa Yanga haujaweka bayana juu ya mchezaji huyo kuondoka.
  Horoya Athletic Club, inayofahamika pia kama Horoya Conakry au H.A.C. ni klabu kongwe Guinea yenye maskani yake mjini Conakry, ambayo ilianzishwa mwaka 1975.
  Na Makambo anaondoka Yanga akiwa kinara wa mabao wa timu hiyo, hadi sasa akiwa ameifungia mabao 17 kwenye Ligi Kuu baada ya kujiunga nayo Juni mwaka jana kutoka St Eloi Lupopo ya kwao, DRC.
  Tayari Yanga SC imesajili wa wachezaji wapya watano, mabeki Mghana, Lamine Moro, Mzanzibari Abdulaziz Makame ambao wote wamewahi kupita kwa mahasimu, Simba SC, winga Patrick ‘Papy’ Sibomana kutoka Mukuta Victory na washambuliaji, Issa Bigirimana kutoka APR za Rwanda na Mzambia Maybin Kalengo kutoka Zesco ya kwao.
  Klabu pia inapambana kukamilisha usajili wa kipa Mkenya, Farouk Shikaro ‘Wazza’ kutoka Bandari ya kwao.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MAKAMBO AWAAGA YANGA SC NA KWENDA KUANZA MAISHA MAPYA HOROYA YA GUINEA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top