• HABARI MPYA

    Thursday, May 10, 2018

    YANGA WAUTEMA RASMI UBINGWA...SIMBA SC WAJIMWAGA KUSHANGILIA TAJI LA KWANZA TANGU 2012

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    RASMI, Simba SC ndiyo mabingwa wapya wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara. Hiyo ni baada ya waliokuwa mabingwa watetezi, Yanga SC kulitema rasmi taji hilo leo, kufuatia kufungwa mabao 2-0 na wenyeji, Tanzania Prisons Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
    Kwa maana hiyo, pointi 65 ambazo wamejikusanyia Simba SC hadi sasa zinawatosha kuitwa mabingwa, kwani Yanga wenye pointi 48 kwa sasa baada ya kucheza mechi 25, hata wakishinda mechi zao zote zilizosalia watafikisha pointi 63 tu.
    Yanga inauachia ubingwa wa Ligi Kuu baada ya kukaa nao kwa misimu mitatu mfululizio wakati, Simba SC inatwaa taji la kwanza la ligi hiyo tangu mwaka 2012 walipochukua kwa mara ya mwisho.
    Katika mchezo wa leo mabao ya Tanzania Prisons yamefungwa na Eliuter Mpepo kwa penalti dakika ya 58 baada ya kiungo Mzimbabwe, Thabani Kamusoko kuushika mpira kwenye boksi na Salum Bosco aliyefunga la pili dakika ya 85 akitumia udhaifu wa mabeki wa Yanga.
    Matokeo haya pia yanamaanisha Yanga SC hawatashiriki michuano ya Afrika mwakani, kwani tayari wametolewa pia na kwenye Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation (ASFC) katika hatua ya Robo Fainali tu.  
    Mechi nyingine ya Ligi Kuu leo, bao pekee la Vincent Philipo dakika ya 45 na ushei limeipa Mbao FC ushindi wa 1-0 dhidi ya Ndanda FC Uwanja wa CCM Kirumba mjiniu Mwanza.
    Kwa ushindi huo, Mbao FC inafikisha pointi 27 baada ya kucheza mechi 27 na kupanda kwa nafasi moja hadi ya 13, wakati Ndanda FC inabaki nafasi ya 15 kwa pointi zake 23 za mechi 28 kwenye Ligi ya timu 16, ambayo timu mbili zitashuka wiki mbili zijazo. 
    Kikosi cha Tanzania Prisons kilikuwa; Aaron Kalambo, Michael Ismail, Laurian Mpalile, Nurdin Chona, James Mwasote/Vedastus Mwahiambi, Jumanne Elfadhil, Benjamin Asukile, Cleophace Mkandala/Adam Kimbongwe, Mohammed Rashid, Ramadhani Ibata/Salum Bosco na Eliuter Mpepo.
    Yanga SC; Benno Kakolanya, Juma Abdul, Emmanuel Martin, Pato Ngonyani, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Maka Edward, Paulo Godfrey/Amissi Tambwe, Thabani Kamusoko, Yohanna Nkomola, Matheo Anthony na Baruan Akilimali/Yussuf Suleiman.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA WAUTEMA RASMI UBINGWA...SIMBA SC WAJIMWAGA KUSHANGILIA TAJI LA KWANZA TANGU 2012 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top