• HABARI MPYA

    Tuesday, May 15, 2018

    SAMATTA AENDA MBALI KUJIPONGEZA KWA KUFUFUA MOTO WA MABAO LIGI YA UBELGIJI

    Na Mwandishi Wetu, GENK
    MSHAMBULIAJI wa kimataifa Tanzania, Mbwana Ally Samatta amekamilisha furaha yake kwa kwenda kupiga picha nzuri eneo la mbali na mji wa Genk kufuatia Jumapili kuifungia mabao mawili KRC Genk katika ushindi wa 4-1 dhidi ya Sporting Charleroi.
    Jumapili Samatta aliendeleza moto wake kwa mabao yake aliyofunga dakika za 24 na 61 katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji Uwanja wa Luminus Arena mjini Genk, wakati mabao mengine ya Genk yalifungwa na Leandro Trossard dakika ya 34 na Dieumerci N'Dongala dakika ya 77.
    Bao la kufutia machozi la  Sporting Charleroi lilifungwa na Cristian Benavente dakika ya 31 katika mchezo ambao Samatta alicheza kwa kiwango kizuri mno.
    Mbwana Samatta amekamilisha furaha yake ya kufufua makali Ubelgiji kwa kwenda kupiga picha eneo la mbali  

    Samatta amefufua makali, baada ya kucheza bila kufunga kwa muda mrefu ‘alifungulia mbwa’ Alhamisi alipotokea benchi na kufungia bao la kusawazisha KRC Genk ikipata sare ya 1-1 na AA Gent katika mchezo wa Ligi pia Uwanja wa Luminus Arena.
    Alhamisi Samatta aliingia uwanjani dakika ya 54 kwenda kuchukua nafasi ya mshambuliaji Mgiriki, Nikolaos Karelis wakati huo tayari Gent wanaongoza kwa 1-0, bao lililofungwa na mshambuliaji kutoka Japan, Yuya Kubo dakika ya 15 akimalizia kazi nzuri ya kiungo kutoka Georgia, Giorgi Chakvetadze.
    Samatta akafunga bao lake dakika ya 66, ambalo lilikuwa la kwanza tangu Oktoba 25, mwaka jana alipofunga bao la pili katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Club Brugge katika Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji, Uwanja wa Luminus Arena pia.
    Lakini Jumapili Samatta alianza na kumaliza mechi akifikisha mabao 25 katika mechi yake ya 88 tangu Nahodha huyo wa Taifa Stars ajiunge na Genk Januari mwaka 2016 akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
    Mbwana Ally Samatta anatarajiwa kuiongoza tena KRC Genk katika mchezo mwingine wa ligi Jumapili ugenini dhidi ya wenyeji, Anderlecht kuanzia Saa 1: 00 usiku Uwanja wa Constant Vanden Stock mjini Brusells.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SAMATTA AENDA MBALI KUJIPONGEZA KWA KUFUFUA MOTO WA MABAO LIGI YA UBELGIJI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top