• HABARI MPYA

    Tuesday, May 15, 2018

    KOCHA AL AHLY AIACHA TIMU KAMPALA BAADA YA KUPIGWA 2-0 NA KCCA

    KOCHA Hossam El-Badry ameng'atuka katika klabu ya Al Ahly kufuatia kipigo cha mabao 2-0 leo mbele ya KCCA ya Uganda kwenye mchezo wa Kundi A Ligi ya Mabingwa Afrika uliofanyika Uwanja wa Nelson Mandela, uliopo Namboole mjini Kampala.
    Uongozi wa Ahly umekubali ombi la kocha huyo mwenye umri wa 58 kujiuzulu na kukamilisha awamu yake ya tatu ya kuwa mwalimu wa timu hiyo bora ya karne Afrika.
    “Kamati ya Soka imekubali uamuzi wa Hossam Al-Badry kujiuzulu,” imesema taarifa ya klabu katika ukurasa wake wa twitter leo jioni.

    Hossam aliingia kwenye mchezo wa leo mjini Kampala tayari alikuwa kwenye presha kufuatia sare ya 0-0 nyumbani dhidi ya jirani zao, Esperance ya Tunisia kwenye mchezo wa ufunguzi wa kundi hilo.
    Lakini mabao ya Saddam Juma dakika ya 73 na Timothy Awany kwa penalti dakika ya 89 leo yamehitimisha zama zake za kuitwa kocha wa Al Ahly.
    Mapema katika mchezo huo, mabingwa hao mara 40 wa Misri walikosa penalti baada ya mkwaju wa Walid Soliman kuokolewa na kipa wa KCCA, Charles Lukwago dakika ya 24.
    Hossam alijiunga tena na Ahly Agosti 2016 kwa mara ya tatu – akichukua nafasi ya Mholanzi mwenye umri wa miaka 62- Martin Jol. 
    Katika awamu yake ya tatu ya kufundisha timu hiyo imetwaa mataji mawili ya Ligi Kuu ya Misri, Kombe la Misri na Super Cup ya Misri mara moja kila moja.
    Lakini akashindwa kuipa Ahly taji muhimu, la Ligi ya Mabingwa wakifungwa kwenye fainali na Wydad Casablanca ya Morocco mwaka jana.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KOCHA AL AHLY AIACHA TIMU KAMPALA BAADA YA KUPIGWA 2-0 NA KCCA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top