• HABARI MPYA

    Monday, May 14, 2018

    RAYON SPORT, MAREFA WAWASILI DAR KUIVAA YANGA JUMATANO UWANJA WA TAIFA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    WAPINZANI wa Yanga katika mchezo wa Jumatano wa Kombe la Shirikisho Afrika, Rayon Sport ya Rwanda wamewasili mchana huu tayari kwa mtanange huo wa Kundi D Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Rayon wamewasili kwa ndege ya kwao, Rwanda Air na kesho watafanya mazoezi Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
    Marefa wa mchezo huo, Helder Martins De Carvalho atakayepulisza filimbi akisaidiwa na washika vibendera Ivanildo Meirelles De O Sanche Lopes na Wilson Valdmiro Ntyamba wote wa Angola nao wanawasili leo.
    Viingilio katika mchezo huo vitakuwa ni Sh. 15,000 kwa VIP A, 7,000 kwa VIP B na C na 3,000 kwa mzunguko.
    Kwa upande wa Yanga, wanarejea leo Dar es Salaam kutoka Morogoro ambako jana walicheza mechi ya Ligi Kuu ys Vodacom Tanzania Bara na kufungwa 1-0 na wenyeji, Mtibwa Sugar Uwanja wa Jamhuri. 
    Kipigo hicho kinazidi kuwaweka Yanga katika mazingira magumu ya kumaliza Ligi Kuu ndani ya nafasi tatu za juu, kwani sasa wakiwa wamecheza mechi 26 wanazidiwa pointi nne na Azam FC walio nafasi ya pili kwa pointi zao 52 za mechi 28.
    Mara ya mwisho Yanga kushinda ilikuwa ni Aprili 7, mwaka huu walipoichapa 2-0 Welayta Dicha ya Ethiopia katika mchezo wa kwanza wa mchujo wa kuwania kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika wakiwa chini ya kocha wao, Mzambia George Lwandamina.
    Baada ya mchezo huo, Lwandamina alipakia mizigo yake kurejea kwao na tangu hapo Yanga hawajashinda tena, katika mechi saba, wakifungwa tano na kutoa sare mbili.
    Yanga ilianza vibaya mechi za makundi Kombe la Shirikisho Mei 6 kwa kufungwa mabao 4-0 na wenyeji, U.S.M. Alger Uwanja wa Julai 5, 1962.
    Michuano ya Kombe la Shirikisho itasimama baada ya mechi za katikati ya wiki hii, Yanga na Rayon na Gor Mahia na USM Alger kupisha Fainali za kombe la Dunia mwezi ujao nchini Urusi. Yanga watakamilisha mechi zao za mzunguko wa kwanza kwa kuwafuata Gor Mahia mjini Nairobi Julai 18.
    Mzunguko wa pili Yanga itaanzia nyumbani Julai 29 na Gor Mahia, kabla ya kuwakaribisha na USMA Alger Agosti 19 na kwenda kumalizia ugenini Agosti 29 na Rayon.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: RAYON SPORT, MAREFA WAWASILI DAR KUIVAA YANGA JUMATANO UWANJA WA TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top