• HABARI MPYA

  Wednesday, May 02, 2018

  NDEMLA AGOMA KUONGEZA MKATABA SIMBA SC, ANAKWENDA ULAYA KAMA MCHEZAJI HURU

  Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
  KIUNGO Said Hamisi Ndemla ataondoka kama Mchezaji Huru Simba SC kwenda kujiunga na AFC Eskilstuna ya Sweden kufuatia kumaliza mkataba wake.
  Ndemla amemaliza mkataba wake Aprili 30, yaani Jumatatu na amekataa kuongeza mkataba mpya kwa kuwa tayari mipango yake ni kwenda AFC Eskilstuna.
  Hata hivyo, Ndemla atalazimika kusubiri hadi msimu ujao ili kuanza kucheza Ligi Kuu ya Sweden kwa kuwa dirisha la usajili limekwishafungwa na msimu unaelekea ukingoni.
  Ndemla angeweza kuanza kucheza AFC Eskilstuna kumalizia msimu kama klabu yake, Simba SC ingekubali ombi la klabu hiyo ya Sweden kumtoa kwa mkopo kumalizia msimu. 
  Said Ndemla anaondoka kama Mchezaji Huru Simba SC kwenda kujiunga na AFC Eskilstuna ya Sweden 

  Mwenyewe Ndemla yupo tayari kwenda kuanza mazoezi na AFC Eskilstuna akisubiri msimu ujao aanze rasmi kazi barani Ulaya.
  Ikumbukwe Ndemla alikwenda kufanya majaribio AFC Eskilstuna mapema Novemba mwaka jana, ambako baada ya kufuzu klabu hiyo ikaingia kwenye mazungumzo na Simba SC.
  Pamoja na kwamba hakukuwa na taarifa zozote juu ya kikao cha Simba SC na viongozi wa AFC Eskilstuna waliotarajiwa kuja nchini baada ya kuridhishwa na uwezo wa Ndemla, lakini tu inaonekana pande hizo mbili hazikufikia maafikiano na itakuwa katika dau la mauziano. 
  Pamoja na kwamba Ndemla ataondoka kama mchezaji huru, lakini itanufaika iwapo kiungo huyo atauzwa na AFC Eskilstuna kwenda klabu nyingine ndipo Wekundu wa Mzimbazi watapata asilimia 20 kwa sababu mchezaji huyo ametokea katika timu ya vijana ya klabu hiyo. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NDEMLA AGOMA KUONGEZA MKATABA SIMBA SC, ANAKWENDA ULAYA KAMA MCHEZAJI HURU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top