• HABARI MPYA

    Tuesday, May 15, 2018

    MECHI YA YANGA NA RAYON KUCHEZWA SAA 1:00 USIKU TAIFA…KIINGILIO 3,000

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MCHEZO wa Kundi D Kombe la Shirikisho Afrika kati ya wenyeji, Yanga SC na Rayon Sport ya Rwanda utaanza Saa 1:00 usiku Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Nahodha wa Yanga SC, Nadir Haroub ‘Cannavaro ’ amesema kwamba wamejipanga vizuri kwa ajili ya mchezo huo na lengo lao ni kushinda ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kwenda Robo Fainali.
    “Tunawafahamu Rayon ni timu nzuri na tunatarajia ushindani mkali, lakini tumejipanga na tumedhairia kushinda,”amesema Cannavaro.
    Katika mchezo huo, Yanga SC watamkosa kiungo wao, Said Juma ‘Makapu’ ambaye atakuwa anatumikia adhabu ya kadi za njano.  
    Nahodha wa Yanga SC, Nadir Haroub 'Cannavaro' (kushoto) akizungumza na Waandishi wa Habari leo 

    Kwa upande wao, Rayon wamesema pia wanawaheshimu Yanga na wanatarajia mchezo mzuri wenye ushindani, lakini watajitahidi washinde.
    Mechi hiyo itachezeshwa na maarefa kutoka Angola, Helder Martins De Carvalho atakayepulisza filimbi akisaidiwa na washika vibendera Ivanildo Meirelles De O Sanche Lopes na Wilson Valdmiro Ntyamba na viingilio ni Sh. 15,000 kwa VIP A, 7,000 kwa VIP B na C na 3,000 kwa mzunguko.
    Yanga itaingia kwenye mechi hiyo ikitoka kucheza mechi saba bila ya ushindi, tangu waliposhinda Aprili 7, mwaka huu walipoichapa 2-0 Welayta Dicha ya Ethiopia katika mchezo wa kwanza wa mchujo wa kuwania kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika wakiwa chini ya kocha wao, Mzambia George Lwandamina.
    Baada ya mchezo huo, Lwandamina alipakia mizigo yake kurejea kwao na tangu hapo Yanga hawajashinda tena, katika mechi saba, wakifungwa tano na kutoa sare mbili.
    Yanga ilianza vibaya mechi za makundi Kombe la Shirikisho Mei 6 kwa kufungwa mabao 4-0 na wenyeji, U.S.M. Alger Uwanja wa Julai 5, 1962 mjini Algiers, Algeria wakati Rayon ililazimishwa sare ya 1-1 na Gor Mahia siku hiyo mjini Kigali.
    Michuano ya Kombe la Shirikisho itasimama baada ya mechi za katikati ya wiki hii, Yanga na Rayon na Gor Mahia na USM Alger kupisha Fainali za kombe la Dunia mwezi ujao nchini Urusi. Yanga watakamilisha mechi zao za mzunguko wa kwanza kwa kuwafuata Gor Mahia mjini Nairobi Julai 18.
    Mzunguko wa pili Yanga itaanzia nyumbani Julai 29 na Gor Mahia, kabla ya kuwakaribisha na USMA Alger Agosti 19 na kwenda kumalizia ugenini Agosti 29 na Rayon.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MECHI YA YANGA NA RAYON KUCHEZWA SAA 1:00 USIKU TAIFA…KIINGILIO 3,000 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top