• HABARI MPYA

    Tuesday, May 15, 2018

    RAIS MAGUFULI AOMBWA KUIKABIDHI SIMBA SC KOMBE JUMAMOSI TAIFA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia amesema kwamba amemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Joseph Magufuli kuwakabidhi Kombe la ubingwa wa Ligi Kuu, Simba SC Jumamosi Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
    Akizungumza na Waandishi wa Habari leo makao makuu ya ofisi za TFF, Uwanja wa Karume, Ilala mjini Dar es Salaam, Karia amesema kwamba wanasubiri majibu kuhusu ombi hilo.
    Pamoja na hayo, Rais Karia amesema kwamba siku hiyo kama Rais Magufuli atakubali mwaliko huo, ataanza kwa kukabidhiwa Kombe la ubingwa wa michuano ya Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 (CECAFA U17), ambalo Tanzania ilitwaa mapema mwezi huu nchini Burundi.
    Rais Dk. John Pombe Joseph Magufuli (kulia) akiwa na mtangulizi wake, Rais wa awamu ya nne, Dk. Jakaya Kikwete

    Simba SC wanatarajiwa kuwaalika Kagera Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Mechi hiyo itakuwa maalum kwa Wekundu hao wa Msimbazi kukabidhiwa taji la ubingwa wa Ligi Kuu walilolitwaa Alhamisi wiki iliyopita baada ya mahasimu wao wa jadi, Yanga SC kufungwa 2-0 na Tanzania Prisons mjini Mbeya.
    Simba SC wakajihakikishia wao ni mabingwa wa nchi baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Singida United Jumamosi Uwanja wa Namfua mjini Singida.
    Simba SC wamekwishajikusanyia pointi 68 hadi katika mechi 28, ambazo kati ya hizo wameshinda 20 na kutoa sare nane na baada ya mchezo wa Jumamosi watakwenda kukamilisha msimu kwa mchezo dhidi ya Maji Maji mjini Songea mkoani Ruvuma. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: RAIS MAGUFULI AOMBWA KUIKABIDHI SIMBA SC KOMBE JUMAMOSI TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top