• HABARI MPYA

  Monday, May 14, 2018

  SAMATTA ‘AFUNGULIA MBWA’ ULAYA…NA LEO KAPIGA MABAO MAWILI GENK IKISHINDA 4-1

  Na Mwandishi Wetu, GENK
  MSHAMBULIAJI wa kimataifa Tanzania, Mbwana Ally Samatta usiku wa Jumapili amecheza muda wote na kuifungia KRC Genk mabao mawili ikiibuka na ushindi wa 4-1 dhidi ya Sporting Charleroi katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji Uwanja wa Luminus Arena mjini Genk.
  Samatta amefufua makali, baada ya kucheza bila kufunga kwa muda mrefu ‘alifungulia mbwa’ Alhamisi alipotokea benchi na kufungia bao la kusawazisha KRC Genk ikipata sare ya 1-1 na AA Gent katika mchezo wa Ligi pia Uwanja wa Luminus Arena.
  Na leo Samatta ameendeleza moto wake kwa mabao yake aliyofunga dakika za 24 na 61, wakati mabao mengine ya Genk yamefungwa na Leandro Trossard dakika ya 34 na Dieumerci N'Dongala dakika ya 77, wakati la kufutia machozi la  Sporting Charleroi limefungwa na Cristian Benavente dakika ya 31.
  Mbwana Samatta ameifungia KRC Genk mabao mawili ikiibuka na ushindi wa 4-1 dhidi ya Sporting Charleroi leo

  Alhamisi Samatta aliingia uwanjani dakika ya 54 kwenda kuchukua nafasi ya mshambuliaji Mgiriki, Nikolaos Karelis wakati huo tayari Gent wanaongoza kwa 1-0, bao lililofungwa na mshambuliaji kutoka Japan, Yuya Kubo dakika ya 15 akimalizia kazi nzuri ya kiungo kutoka Georgia, Giorgi Chakvetadze.
  Samatta akafunga bao lake dakika ya 66, ambalo lilikuwa la kwanza tangu Oktoba 25, mwaka jana alipofunga bao la pili katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Club Brugge katika Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji, Uwanja wa Luminus Arena pia.
  Lakini leo Samatta ameanza na kumaliza mechi akifikisha mabao 25 katika mechi yake ya 88 tangu Nahodha huyo wa Taifa Stars ajiunge na Genk Januari mwaka 2016 akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
  Kikosi cha KRC Genk kilikuwa; Vukovic, Nastic, Colley, Aidoo, Mata, Wouters, Malinovskyi, Pozuelo/Writers dk82, Trossard/Zhegrova dk82, Ndongala/Buffel dk76 na Samatta.
  Charleroi : Penneteau, Martos, Rezaei, Benavente, Marinos, Baby, Hendrickx/Bedia dk70, Dessoleil, Ilaimaharitra, N'Ganga/Nurio dk70 na Fall/Grange dk60.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SAMATTA ‘AFUNGULIA MBWA’ ULAYA…NA LEO KAPIGA MABAO MAWILI GENK IKISHINDA 4-1 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top