• HABARI MPYA

    Monday, July 23, 2012

    YANGA WASAKA NUSU FAINALI LEO


    Kikosi cha Yanga kilichoipiga APR 2-0

    Na Prince Akbar
    MABINGWA watetezi wa Klabu Bingwa ya soka Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, Yanga SC ya Dar es Salaam, leo wanashuka dimbani kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kumenyana na Mafunzo ya Zanzibar katika hatua ya Robo Fainali ya michuano hiyo.
    Kocha wa Yanga, Mbelgiji Tom Saintfiet katika mchezo wa leo, atamkosa kiungo Nizar Khalfan ambaye anasumbuliwa na maradhi ya nyonga, wakati hali ya kinara wa mabao wa timu hiyo, Said Bahanuzi ‘Spider Man’ hadi jana haikuwa ya kumpa uhakika wa kucheza mechi hiyo.
    Bahanuzi anasumbuliwa na maumivu ya mgongo, wakat kiungo Nizar Khalfan yeye kwa asilimia 100 hatacheza kutokana na maumivu hayo ya nyonga.
    Saintfiet aliiambia BIN ZUBEIRY jana kwamba, Nizar hatacheza kabisa, lakini wachezaji wengine watatu, Bahanuzi,  kipa Yaw Berko anayesumbuliwa na goti, kiungo Athumani Iddi ‘Chuji’ na Hamisi Kiiza wanaosumbuliwa na quadriceps wako kwenye hatihati kucheza.
    Mtakatifu Tom amesema kwamba, Daktari wa Yanga, Sufiani Juma anaendelea kufuatilia kwa karibu hali za Bahanuzi, Kiiza, Berko na Chuji ili kuhakikisha wanakuwa fiti kwa ajili ya mechi ya leo.
    Amesema sababu ya wachezaji wake kuumia mara kwa mara ni kutokana na kucheza mechi mfululizo na kulingana na kanuni za mashindano hayo, hawezi kutumia wachezaji zaidi ya 20, hivyo hana namna nyingine zaidi ya kupambana na hali hiyo.
    Bahanuzi ndiye kinara wa mabao wa Yanga hivi sasa, hadi sasa akiwa amekwishaifungia timu hiyo mabao manne, hivyo kuingia kwenye mbio za kuwania kiatu cha dhahabu cha mashindano hayo, ambayo tayari kwenye kabati la Yanga kuna mataji manne yamehifadhiwa.
    Mshambuliaji huyo mpya kutoka Mtibwa Sugar ya Morogoro, Ijumaa alikaribia kuondoka na mpira uwanjani, kama si refa Dennis Batte kutoka Uganda kukataa bao lake moja siku ambayo alifunga mawili yaliyokubaliwa dhidi ya APR ya Rwanda, Yanga ikishinda 2-0, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jioni hii.
    Katika mchezo huo, Kocha Tom alimpumzisha Bahanuzi dakika ya 72 na nafasi yake ikachukuliwa na Jerry Tegete, wakati Nizar Khalfan kabla ya hapo alimpisha Juma Seif ‘Kijiko’.
    Matatizo ya mgongo kwa Spider Man
    yalianzia kwenye mechi na APR
    Mchezo kati ya Yanga na Mafunzo, utaanza saa 10:00 jioni na utatanguliwa na mechi nyingine ya Robo Fainali kati ya URA ya Uganda na APR ya Rwanda, wakati kesho Atletico Olympique Sport ya Burundi itamenyana na AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) katika Robo ya Fainali ya tatu mchana, kabla ya Azam FC na Simba SC, zote za Dar es Salaam, kuhitimisha awamu ya Nane Bora ya michuano hiyo.
    Michuano hii, iliyoanza Julai 14 na inatarajiwa kufikia tamati Julai 28, inadhaminiwa na Azam na SuperSport Televisheni.

    RATIBA ROBO FAINALI
    Julai 23, 2012
    URA vs APR (Saa 8:00 mchana)
    Mafunzo vs Yanga (Saa 10:00 jioni)
    Julai 24, July
    Atletico vs AS Vita (Saa 8:00 mchana)
    Azam vs Simba SC (Saa 10:000 jioni)
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA WASAKA NUSU FAINALI LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top