• HABARI MPYA

  Tuesday, July 24, 2012

  NILIWAAGIZA VIJANA WANGU WACHEZE TARATIBU, ASEMA MTAKATIFU TOM


  Mtakatifu Tom, akiwa na Kombe la Kagame

  Na Prince Akbar
  KOCHA wa Yanga, Mbelgiji Tom Saintfiet amesema kwamba aliwaelekeza vijana wake kucheza kwa kutotumia nguvu nyingi katika mchezo wa jana dhidi ya Mafunzo, kwani alijua watakuwa na mechi nyingine ngumu baada ya siku moja katika Nusu Fainali.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY baada ya mechi ya Robo Fainali dhidi ta Mafunzo ya Zanzibar jana, Mtakatifu Tom alisema kwamba vijana wake wamecheza kwa kufuata maelekezo yake na hakutaka ushindi mkubwa jana, bali ushindi tu.
  Hata hivyo, anasikitika kuumia kwa kipa wake namba moja, Mghana Yaw Berko katika mchezo huo, kwani kunaiathiri timu yake.
  “Wachezaji wanaumia sana kwa sababu mechi zipo karibu karibu mno, hakuna jinsi zaidi ya kuendelea kukabiliana na hali hii,”alisema.
  Aidha, Tom alisema kwamba hakupenda kabisa kukutana tena na APR katika Nusu Fainali kwa sababu amekwishakutana nao kwenye kundi lake, C zaidi alitarajia changamoto mpya kutoka URA ya Uganda.
  “Lakini kwa kuwa tupo kwenye mashindano, tunakabiliana na timu yoyote. Nawaheshimu APR, ni timu nzuri na hatukuwafunga kwa urahisi kwenye mechi ya kwanza, utakuwa mchezo mgumu sana,”alisema Tom.
  Yanga jana imefuzu kuingia Nusu Fainali ya Kombe la Kagame, baada ya kuifunga Mafunzo ya Zanzibar kwa penalti 5-3, kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 90 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Wawakilishi wa Zanzibar Mafunzo walikuwa wa kwanza kupata bao lililofungwa na Ali Othman Mmanga, dakika ya 34, akiunganisha kona ya Juma Othman Mmanga na Yanga wakasawazisha dakika ya 46, mfungaji Said Bahanuzi ‘Spider Man’.
  Yanga sasa kesho itamenyana na APR ya Rwanda, ambayo katika Robo Fainali ya kwanza, iliitoa URA ya Uganda kwa kuifunga mabao 2-1, mabao yake yakifungwa na Jean Claude Iranzi dakika ya tisa na Suleiman Ndikumana dakika ya 34, wakati la Watoza Ushuru wa Kampala, lilifungwa na Robert Ssentongo dakika ya 57.
  Kipa wa Yanga Berko aliumia dakika ya 69 na akatibiwa kwa dakika tatu, kabla ya kutolewa nje dakika ya 72, nafasi yake ikichukuliwa na Ally Mustafa Barthez ambaye ukaaji wake mazuri langoni wakati wa penalti ulimfanya Said Mussa Shaaban wa Mafunzo akapiga nje na kuipa Yanga ushindi.
  Nyota wa Mafunzo, Juma Othman Mmanga alipoteza fahamu na kuwaweka roho juu wachezaji wenzake na mashabiki, akatolewa nje akipepewa na hakuweza kuendelea na mchezo, lakini taarifa za baada ya mchezo zilisema anaendelea vizuri.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NILIWAAGIZA VIJANA WANGU WACHEZE TARATIBU, ASEMA MTAKATIFU TOM Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top