• HABARI MPYA

    Monday, July 30, 2012

    ACHAJI GERO AOMBA KAZI, AZAM, SIMBA


    Achaji Gero

    Na Prince Akbar
    MSHAMBULIAJI wa Enugu Rangers ya Nigeria, Achaji Gero amesema kwamba yuko tayari kujiunga klabu yoyote ya Ligi Kuu ya Tanzania, lakini atatazama mambo mawili tu- maslahi bora na hadhi ya timu, lazima iwe inayocheza michuano ya Afrika.
    Gero aliyeiongoza Flying Eagles kuifunga timu ya taifa ya vijana ya Tanzania chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro Heroes mabao 2-1 jana katika mechi ya kwanza ya Raundi ya Pili, kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika, amesema kama atapata timu itakayomlea vizuri na pia inacheza michuano ya Afrika anaamini anaweza kutimiza ndoto zake za kucheza Ulaya.
    Mshambuliaji huyo mrefu wa Enugu Rangers, aliyefunga mabao yake katika dakika ya pili na 44 jana, aliwavutia wengi miongoni mwa watazamaji waliojitokeza uwanjani kutokana na soka yake ya maridadi.
    Katika mchezo huo, kipindi cha pili, Ngorongoro walibadilika na kucheza vizuri, wakiwazidi wapinzani wao kumiliki mpira na kasi ya mchezo na hatimaye wakafanikiwa kupata bao la kufutia machozi, lililofungwa na Atupele Green dakika ya 50, akimalizia krosi ya Ramadhani Singano ‘Messi’.
    Ngorongoro wangeweza kupata mabao zaidi, kama wangecheza soka ya chini, lakini kutia krosi za juu kwenye lango la Nigeria ilikuwa ni kuwatesa washambuliaji wao wafupi, Atupele na Simon Msuva.
    Kwa matokeo hayo sasa, Ngorongoro wanahitaji ushindi wa angalau wa mabao 2-0 katika mchezo wa marudiano Nigeria wiki mbili zijazo, ili kusonga mbele.
    Baada ya mchezo huo, kocha wa Ngorongoro Heroes, Mdenmark Jakob Michelsen alisema kwamba ataongeza nguvu katika kikosi chake kwa kuwaita wachezaji wawili wanaocheza nje, kiungo Adam Nditi wa Chelsea na Thomas Ulimwengu wa Tout Puissant Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), sambamba na nyota wengine waliokwenda Ujerumani n TSU kwenye michuano ya Fallerhof.
    Huo ulikuwa mchezo wa tatu mfululizo, Ngorongoro inafungwa nyumbani tangu Michelsen aanze kuifundisha timu hiyo, akirithi mikoba ya Kim Poulsen, Mdenmark mwenzake, ambaye amepandishwa timu ya wakubwa, baada ya awali wiki mbili zilizopita kufungwa na Rwanda mara mbili Dar es Salaam.
    Katika mchezo, kikosi cha Ngorongoro kilikuwa; Barwany Khomein, Omega Seme, Jamal Mroki, Issa Rashid, Ruhana Samir, Yarouk Ramadhan, Kheri Salum/Jerome Lambele, Frank Damayo, Simon Msuva, Atupele Green na Ramadhan Singano.
    Flying Eagles; Samuel Okani, Hassan Abubakar, Ahiyu Mohamed, Ikechukwu Okine, Chizoba Amaefule, Agboyi Oubokha, Moses Orkuma, Chidi Osochukwu, Yahaya Adam/Harrison Egbune, Achaji Gero na Aminu Omar/Uchw Agbo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: ACHAJI GERO AOMBA KAZI, AZAM, SIMBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top