• HABARI MPYA

    Monday, July 23, 2012

    WIKI MBILI KUAMUA HATIMA YA OKWI BUNDESLIGA


    Okwi

    Na Princess Asia
    EMMANUEL Okwi, mshambuliaji wa Simba SC amepewa wiki mbili zaidi za kuendelea na majaribio katika klabu ya FC Red Bull Salzburg ya Austria yenye maskani yake Wals-Siezenheim, nchini humo na baada ya hapo ndipo majibu yatatoka.
    Katibu wa Simba Evodius Mtawala ameiambia BIN ZUBEIRY jana usiku kwamba, Okwi ambaye tayari yuko huko kwa wiki moja, hadi sasa anafanya vizuri ndio maana kapewa wiki mbili zaidi, ili kocha wa klabu hiyo ajiridhishe zaidi na kiwango cha Mganda huyo.
    Klabu hiyo inayotumia Uwanja wa Red Bull Arena, ikiwa zaidi inafahamika kama SV Austria Salzburg kabla haijanunuliwa na kampuni ya Red Bull mwaka 2005, imewahi kufika Fainali ya Kombe la UEFA mwaka 1994 na inacheza Ligi Kuu ya Austria, iitwayo Bundesliga kama Ligi Kuu ya Ujerumani.
    Timu hiyo ni kama timu ambayo Okwi, anachezea kwa sasa, Simba SC, kwani nayo inavaa jezi za rangi ya nyeupe na nyekundu na imewahi kutwaa taji la Bundesliga ya Austria mara saba na pia ilicheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu wa 1994–1995 kama Casino Salzburg, na kuwa timu pekee, ambayo haikufungwa na mabingwa wa wakati huo, Ajax Amsterdam.
    Awali, Okwi aliikosesha Simba Sh. Bilioni 2 kwa kukataa kujiunga na klabu ya Mamelodi Sundown ya Afrika Kusini na kuamua kwenda Austria, ambako inaelezwa klabu hiyo iko tayari kutoa Euro 600,000 akifuzu.
    Awali Olando Pirates ya Afrika Kusini ilimuomba Okwi akafanye majaribio huko kama angefuzu wangemsajili dau la dola 550,000 kabla ya kuibuka kwa taarifa za kutakiwa Italia na klabu ya Parma.
    Hata hivyo, Simba SC ilisema imeshindwa kumshawishi Okwi kwenda kucheza Afrika Kusini kwa kuwa mwenyewe anataka kucheza Ulaya tu. Wakala aliyeiunganisha Simba na Pirates akawasilisha ofa nyingine kutoka Mamelodi, ambayo ni Euro 600,000 na kupanda hadi Sh. Bilioni 2, lakini bado mabingwa hao wa Tanzania, walishindwa kumshawishi Okwi kwenda Ligi Kuu ya Afika Kusini (PSL).
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: WIKI MBILI KUAMUA HATIMA YA OKWI BUNDESLIGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top