• HABARI MPYA

  Friday, July 27, 2012

  MTAKATIFU TOM; KWELI AZAM WAZURI, LAKINI KOMBE HALIBANDUKI JANGWANI


  Mtakatifu Tom, akiwa na Kombe la Kagame, siku alipotua tu Jangwani

  Na Prince Akbar
  KOCHA wa Yanga, Tom Saintfiet amesema kwamba fainali ya Klabu Bingwa ya soka Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame itakuwa ngumu kwa sababu wapinzani wao, Azam FC ni timu yenye kucheza kandanda ya kuvutia.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY leo, baada ya kujikatia tiketi ya fainali kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya APR ya Rwanda, Mbelgiji huyo alisema kwamba ana majeruhi wengi kikosini na ilipofikia ni kama hana wachezaji wa akiba kwa sababu ya wachezaji wengi kuumia.
  Hata hivyo, Mtakatifu Tom amesema kwamba pamoja na ukweli huo wanahitaji kutetea Kombe na watapigana hivyo hivyo pamoja na changamoto zinazowakabili kuhakikisha taji linabaki nyumbani.
  Yanga imefuzu kuingia Fainali, jana baada ya kuifunga APR 1-0, bao pekee la mwanasoka bora wa Uganda, Hamisi Kiiza ‘Diego’ dakika ya 110 na sasa itamenyana na Azam FC keshokutwa, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Kiiza alifunga bao hilo, kwa kichwa akiunganisha krosi ya karibu ya Haruna Niyonzima ambaye alitumia mwanya wa mabeki wa APR kuzubaa wakisikilizia maamuzi ya refa, baada ya Said Bahanuzi kuangushwa.
  Yanga waliinuka na wakaanzisha shambulizi la haraka lililozaa bao hilo. Dakika tatu baada ya bao hilo, beki wa Yanga, Godfrey Taita alitolewa nje kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja na sasa ataikosa fainali.
  Ikumbukwe mwaka jana, Yanga iliifunga Simba SC katika fainali bao 1-0 na kutwaa taji la nne la michuano hiyo, baada ya awali kutwaa Kombe hilo 1975, 1993 na 1999.
  Mapema katika Nusu Fainali ya Kwanza, Azam FC iliitoa AS Vita kwa kuifunga mabao 2-1, mabao yake yakifungwa na John Bocco ‘Adebayor’ na Mrisho Ngassa, wakati la Vita ya DRC lilifungwa na Mfongang Alfred.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MTAKATIFU TOM; KWELI AZAM WAZURI, LAKINI KOMBE HALIBANDUKI JANGWANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top