• HABARI MPYA

    Thursday, July 26, 2012

    MESSI AMFUATA OKWI AUSTRIA, SIMBA KULAMBA DOLA 300,000


    Messi wa Msimbazi; Rama Singano

    Na Princess Asia
    KIUNGO chipukizi wa Simba SC, Ramadhani Singano ‘Messi’ anatarajiwa kuondoka nchini wakati wowote kwenda Austria kwa majaribio ya soka ya kulipwa, imeelezwa.
    Chanzo cha habari cha uhakika kutoka ndani ya Simba SC, kimeiambia BIN ZUBEIRY jana kwamba, Messi amepata ofa hiyo ya majaribio kupitia wakala mmoja wa wachezaji Tanzania, anayetambuliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), anayefanya kazi na klabu hiyo.
    “Kuna wakala mmoja ambaye anafanya kazi na sisi, ameleta ofa hiyo na kama kijana atafuzu, Simba itapata kama dola za Kimarekani 300,000 hivi,”kilisema chanzo kutoka Simba SC.
    Messi huyo alipandishwa kutoka timu ya vijana ya Simba msimu uliopita na pamoja na kuingia mara chache akitokea benchi, lakini amewavutia wengi kwa soka yake na kwa sasa ni miongoni mwa wachezaji tegemeo wa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro Heroes. 
    Tayari mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi, anaendelea na majaribio katika klabu ya FC Red Bull Salzburg ya Austria yenye maskani yake Wals-Siezenheim, nchini humo na baada ya hapo ndipo majibu yatatoka.
    Klabu hiyo inayotumia Uwanja wa Red Bull Arena, ikiwa zaidi inafahamika kama SV Austria Salzburg kabla haijanunuliwa na kampuni ya Red Bull mwaka 2005, imewahi kufika Fainali ya Kombe la UEFA mwaka 1994 na inacheza Ligi Kuu ya Austria, iitwayo Bundesliga kama Ligi Kuu ya Ujerumani.
    Timu hiyo ni kama timu ambayo Okwi, anachezea kwa sasa, Simba SC, kwani nayo inavaa jezi za rangi ya nyeupe na nyekundu na imewahi kutwaa taji la Bundesliga ya Austria mara saba na pia ilicheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu wa 1994–1995 kama Casino Salzburg, na kuwa timu pekee, ambayo haikufungwa na mabingwa wa wakati huo, Ajax Amsterdam.
    Awali, Okwi aliikosesha Simba Sh. Bilioni 2 kwa kukataa kujiunga na klabu ya Mamelodi Sundown ya Afrika Kusini na kuamua kwenda Austria, ambako inaelezwa klabu hiyo iko tayari kutoa Euro 600,000 akifuzu.
    Awali Orlando Pirates ya Afrika Kusini ilimuomba Okwi akafanye majaribio huko kama angefuzu wangemsajili dau la dola 550,000 kabla ya kuibuka kwa taarifa za kutakiwa Italia na klabu ya Parma.
    Hata hivyo, Simba SC ilisema imeshindwa kumshawishi Okwi kwenda kucheza Afrika Kusini kwa kuwa mwenyewe anataka kucheza Ulaya tu. Wakala aliyeiunganisha Simba na Pirates akawasilisha ofa nyingine kutoka Mamelodi, ambayo ni Euro 600,000 na kupanda hadi Sh. Bilioni 2, lakini bado mabingwa hao wa Tanzania, walishindwa kumshawishi Okwi kwenda Ligi Kuu ya Afika Kusini (PSL).

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MESSI AMFUATA OKWI AUSTRIA, SIMBA KULAMBA DOLA 300,000 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top