• HABARI MPYA

  Friday, July 20, 2012

  YANGA SASA INATISHA, YAWACHAPA APR 2-0 KAMA WAMESIMAMA, SHUJAA BAHANUZI


  OGOPA JEZI NAMBA 11 YANGA; Said Bahanuzi akishangilia kwa staili ya kuonyesha jezi namba yake baada ya kufunga bao leo

  Na Prince Akbar
  YANGA imeonyesha matumaini ya kutetea taji lake la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, baada ya kuifunga APR ya Rwanda mabao 2-0, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jioni hii.
  Shujaa wa Yanga leo, alikuwa ni mshambuliaji mpya kutoka Mtibwa Sugar ya Morogoro, Said Bahanuzi, aliyefunga mabao yote hayo, moja kila kipindi.
  Hadi mapumziko, tayari Yanga ilikuwa mbele kwa bao 1-0, lililofungwa na Bahanuzi dakika ya 22, akiunganisha krosi ya Hamisi Kiiza.
  Dakika ya 43, Bahanuzi alitupia tena mpira nyavuni, pasi ya Kiiza, lakini refa Dennis Batte kutoka Uganda akakataa.
  Kipindi cha pili, Yanga waliendelea kucheza kwa kuelewana na kasi, wakilitia misukosuko muda wote lango la APR na dakika ya 67, beki mmoja wa APR alikuwa anataka kumpiga chenga Bahanuzi kwenye eneo la hatari, lakini mshambuliaji huyo akafanikiwa kuunasa mpira huo na kumtoka beki huyo kabla ya kumchambua kipa Jean Claude Ndoli.
  Lilikuwa bao tamu, ambalo liliwanua vitini mashabiki wa Yanga na kuamini sasa wameshinda mechi.
  Kocha Tom Saintfiet alimpumzisha Bahanuzi dakika ya 72 na nafasi yake ikachukuliwa na Jerry Tegete, wakati Nizar Khalfan kabla ya hapo alimpisha Juma Seif ‘Kijiko’.
  Kwa ushindi huo, Yanga imemaliza mechi za Kundi C ikiwa katika nafasi ya pili kwa pointi zake sita, mabao tisa ya kufunga, matatu ya kufungwa, Bahanuzi akiwa amefunga manne kati ya hayo, akifuatiwa na Hamisi Kiiza mwenye matatu, moja Stefano Mwasyika na lingine Nizar Khalfan.
  Atletico ya Burundi inaendelea kuongoza Kundi C, kwa pointi zake saba, baada ya kucheza mechi tatu, kushinda mbili na kutoa sare moja, wakati APR ya Rwanda inashika nafasi ya tatau nayo imefuzu Robo Fainali, kwa pointi zake nne, wakati Waw Salaam ambayo haina pointi na imeaga.
  Katika mchezo huo, kikosi cha Yanga kilikuwa; Yaw Berko, Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Athumani Iddi ‘Chuji’, Stefano Mwasyika, Haruna Niyonzima, Said Bahanuzi/Jerry Tegete, Hamisi Kiiza na Nizar Khalfan/Juma Seif.
  A.P.R.;  Jean Claude Ndoli, Mbuyu Twite, Kabange Twite, Mugiraneza Jean, Leonel St Preus, Johnson Bagoole, Iranzi Jean Claude, Ngabo Albert, Tuyizere Donatien, Suleiman Ndikumana na Olivier Karekezi.
  Nahodha Cannavaro akimpongeza kijana

  Kiiza akiwa amembeba juu Bahanuzi kumpongeza

  MKALI; Bahanuzi anakwenda kufunga la pili

  HATARI LAKINI SALAM; Kiiza alikosa bao la wazi hapa

  Daktari wa Yanga, Sufiani Juma akimtibu Bahanuzi baada ya kuumizwa na kipa wa APR, Jean Claude Ndoli

  MIPANGO YA KWENYE KONA; Wachezaji wa Yanga wakipiga mishemishe zao langoni mwa APR wakati wa kona

  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA SASA INATISHA, YAWACHAPA APR 2-0 KAMA WAMESIMAMA, SHUJAA BAHANUZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top