• HABARI MPYA

  Thursday, July 26, 2012

  MILOVAN ASEPA KWAO, COSTA, HARUNA WATUPIWA VIRAGO, SIMBA YASAKA MASHINE MPYA ZA UHAKIKA


  Profesa Milovan Cirkovick

  Na Prince Akbar
  WAKATI kocha Mserbia Milovan Cirkovick ameondoka kurejea kwao kwa mapumziko mafupi, klabu ya Simba inasaka beki wa kati, beki wa kulia, beki wa kushoto na mshambuliaji mmoja, lakini wote watakuwa wachezaji wazawa, imeelezwa.
  Habari za ndani kutoka Simba SC, zimesema kwamba baada ya kutolewa katika Klabu Bingwa ya soka Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, pamoja na kugundua hawakuwa na maandalizi ya kutosha, lakini pia wamebaini mapungufu kikosini.
  “Tunahitaji beki wa kulia mmoja, kwa kuwa kipindi hiki beki wetu mwingine wa kulia Chollo (Nassor Masoud) ni majeruhi, anabaki Kapombe (Shomary) pekee, tunahitaji beki wa kushoto, kwa sababu Amir Maftah ni majeruhi pia, anabaki Paul Ngalema pekee. Tayari mchakato umeanza,”kilisema chanzo kutoka Simba SC.
  Aidha, chanzo hicho kimesema Simba pia inasaka beki wa kati mzalendo, kwa kuwa mabeki wake wa kati iliyonao kwa sasa, Lino Masombo, Juma Nyosso na Obadia Mungusa wote ni wa aina moja, hivyo wanasaka beki wa aina tofauti na hao.
  Alisema Simba inaendelea pia kusaka mshambuliaji mwingine mzawa kuongeza nguvu kwenye safu hiyo ambayo hadi sasa inao Felix Mumba Sunzu, Danny Mrwanda na Abdallah Juma.
  “Kama tutamuuza Okwi (Emmanuel) ina maana tutaweza kusajili mshambuliaji mwingine wa kigeni na kwa kweli mrithi wa Okwi lazima Okwi mwingine au zaidi ya Okwi, kwa sababu hadi sasda katika mashindano haya (Kagame) hatujaona mchezaji wa kiwango cha Okwi,”kilisema chanzo hicho.      
  Okwi, anaendelea na majaribio katika klabu ya FC Red Bull Salzburg ya Austria na majibu yake yanatarajiwa kutolewa wiki ijayo na iwapo atafuzu, Simba italipwa Euro 600,000.
  Simba ilitolewa juzi katika Robo Fainali ya Klabu Bingwa ya soka Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, baada ya kufungwa na Azam FC mabao 3-1, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Mbaya wa Simba juzi alikuwa John Raphael Bocco ‘Adebayor’ aliyefunga mabao yote matatu, wakati bao la kufutia machozi la Simba lilifungwa na Shomary Kapombe.
  Wachezaji wote wa Simba wamepewa likizo ya wiki moja na kocha Profesa Milovan Cirkovick anarejea kwao Serbia kwa mapumziko mafupi atarejea wiki ijayo kuendelea na kazi.
  Profesa Milovan akirejea ataanza kuandaa timu kwa ajili ya msimu mpya wa Ligi Kuu, na kikosi kipya cha Simba iliyoboreshwa kitaonekana kwa mara ya kwanza katika tamasha la kila mwaka la kuazimisha kuzaliwa kwa klabu hiyo, Simba Day, ambalo na mwaka huu tena litafanyika Agosti 8, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Wakati huo huo; Habari zaidi kutoka Simba SC zinasema kwamba, iwapo URA haitamnunua beki Haruna Shamte, basi atatolewa tena kwa mkopo kwa kuwa hajamvutia kocha Milovan kwa uchezaji wake. Aidha, Victor Costa naye ametemwa rasmi na yuko huru kujiunga na timu nyingine yoyote.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MILOVAN ASEPA KWAO, COSTA, HARUNA WATUPIWA VIRAGO, SIMBA YASAKA MASHINE MPYA ZA UHAKIKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top