• HABARI MPYA

    Sunday, July 22, 2012

    DULLAH MABAO FITI KUWAVAA AZAM


    Dullah Mabao

    Na Princess Asia
    MSHAMBULIAJI mpya wa Simba na anayeinukia vizuri, aliyeumia kwenye mechi ya jana ya mwisho ya Kundi A, dhidi ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC),  Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Abdallah Juma anaendelea vizuri na anaweza kucheza Nusu Fainali dhidi ya Azam FC Jumatano.
    Dullah Mabao aliumia misuli ya paja la kushoto kwa nyuma dakika ya 27 na kushindwa kuendelea na mchezo huo ulioisha kwa sare ya 1-1, nafasi yake ikichukuliwa na Kiggi Makassy.
    Daktari wa Simba SC, Cossmas Kapinga ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba  Dullah anaendelea vizuri na alipata matatizo kidogo tu ya misuli na kwamba leo anaweza kufanya mazoezi mepesi kujiandaa na Nusu Fainali ya kukata na shoka dhidi ya Azam.
    Pamoja na kutoa sare ya 1-1 na Vita jana, lakini Simba ingeweza kuondoka na ushindi, kama mshambuliaji wake Mzambia, Felix Sunzu asingekosa penalti dakika ya kwanza ya muda wa nyongeza baada ya kutimu dakika 90 za kawaida, kufuatia beki mmoja wa Vita kuunawa mpira kwenye eneo la hatari, lakini shuti lake lilipanguliwa na kipa Mcameroon, Lukong Nelson kabla ya mabeki wake ‘kuosha’.
    Hadi mapumziko, Vita walikuwa mbele kwa bao 1-0, lilifungwa kwa penalti na Etikiama Taddy, dakika ya 35, baada ya Juma Said Nyosso kuunawa mpira kwenye eneo la hatari.
    Simba ilisawazisha bao hilo kupitia kwa Haruna Moshi ‘Boban’ aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Patrick Kanu Mbivayanya dakika ya 66.
    Kwa matokeo hayo, Simba imemaliza kama mshindi wa tatu katika Kundi A na itamenyana na Azam katika Robo Fainali, wakati mabingwa watetezi Yanga watamenyana na Mafunzo Jumanne. Robo Fainali nyingine zitakuwa kati ya URA na APR na Atletico dhidi ya Vita. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: DULLAH MABAO FITI KUWAVAA AZAM Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top