• HABARI MPYA

  Friday, July 27, 2012

  AZAM, YANGA, BAHANUZI, SURE BOY WAMKUNA TENGA


  Tenga kulia akiwa na Jellah Mtagwa, pacha wake enzi hizo Taifa Stars

  Na Prince Akbar
  MWENYEKITI wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Leodegar Chillah Tenga amefurahishwa na kiwango kilichoonyeshwa na timu za nyumbani jana hadi kukata tiketi ya kuingia fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY baada ya mechi za jana, Tenga, ambaye pia ni rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), alisema kwamba ni jambo la kujivunia kwa wenyeji kutumia vema fursa ya kucheza nyumbani kwa kubakiza Kombe nyumbani,”alisema.
  Tenga alisema kwamba kwa kuwa hii inakuwa mara ya pili mfululizo kwa klabu za Tanzania kukutana kwenye fainali, anaamini sasa ushindani utaongezeka kwenye michuano hiyo na kama kuna watu wataamini hiyo inatokana na uenyeji, basi anaamini nchi nyingine zitaomba uenyeji wa michuano hiyo kuanzia mwakani.
  “Kama watu wataona Tanzania wametumia vema fursa ya kuwa wenyeji, basi na wao watataka kutumia fursa hiyo. Lakini tukirudi nyuma, mwaka 2005, mwaka 2006 na 2008, tulikuwa wenyeji pia na hatuweza kubakiza Kombe nyumbani. Hii maana yake kwa kiasi fulani soka yetu imepanda,”alisema Tenga.
  Lakini pia, rais huyo wa TFF na Nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, alisema kwamba anajivunia pia vipaji vipya vilivyoibuka kwenye michuano hiyo kama Said Bahanuzi wa Yanga ambaye anawania kiatu cha dhahabu cha michuano hiyo.
  Lakini pia, Tenga amefurahishwa na kiwango kilichoonyeshwa na wachezaji chipukizi katika mashindano haya kama Khamisi Mcha ‘Vialli’, Juma Abdul, David Luhende, Salum Abubakar, Abdallah Juma na wengineo.
  “Tumeona, tumeridhishwa na ni hatua nzuri kwa kweli ya kujivunia, sasa tunatarajia fainali bora sana, tunatarajia soka ya kistaarabu na ya kiufundi, tukizingatia timu zote zina makocha weledi na wazoefu,”alisema beki huyo wa kati wa zamani wa Yanga na Pan African.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: AZAM, YANGA, BAHANUZI, SURE BOY WAMKUNA TENGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top