• HABARI MPYA

  Saturday, July 21, 2012

  JEBA AWATENDA SIMBA, AREJEA AZAM NA KUONGEZA MKATABA


  Ibrahim Rajab Jeba

  Na Prince Akbar
  SIMBA SC wanalo mwaka huu. Walimsajili Ibrahim Rajab Jeba wa Azam na akajiunga nao, lakini hivi unaposoma habari hii, mchezaji huyo jana ameongeza mkataba wa mwaka mmoja kuendelea kuwachezea ‘Watoto wa Chamazi’ na tayari amerejea rasmi kwenye klabu hiyo, inayomilikiwa na Said Salim Bakhresa na familia yake.
  Hii inakuja katika wakati ambao, Simba ina machungu ya kupokonywa beki wake, Kevin Yondan aliyehamia Yanga, wakati inadai bado ina mkataba naye.
  Msemaji wa Azam FC, Jaffar Iddi Maganga ameiambia BIN ZUBEIRY leo asubuhi kwamba, Jeba alikwenda kuzungumza na uongozi wa Azam jana akaomba radhi kwa kitendo chake cha kuukiuka mkataba wake na kuomba kurejeshwa kundini.
  “Kwa kweli uongozi umemsamehe kabisa na amerejeshwa kundini na hivi navyozungumza na wewe yuko kwenye himaya ya Azam. Mkataba wake wa sasa unaisha Desemba mwaka huu, lakini jana hiyo hiyo ameongeza mkataba na Azam hadi 2013,”alisema mtangazaji huyo wa zamani wa Radio One na ITV, aliyewahi kuandikia pia gazeti la Nipashe.
  Jeba aliibukia katika akademi ya Azam FC na msimu uliopita alitolewa kwa mkopo Villa Squad ya Kinondoni, ili akapate uzoefu wa Ligi Kuu, hata hivyo kwa bahati mbaya aliumia na hakucheza ligi, lakini mwishoni mwa msimu, Simba SC wakamsajili.
  Hata hivyo, uliibuka mvutano mkubwa baina ya klabu hizo mbili, Azam ikilalamika kupokonywa mchezaji kimabavu na Simba SC, lakini ajabu mchezaji huyo Wekundu wa Msimbazi hawakumtumia kabisa hata kwenye mechi za kirafiki hadi jana anarejea Chamazi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: JEBA AWATENDA SIMBA, AREJEA AZAM NA KUONGEZA MKATABA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top