• HABARI MPYA

    Tuesday, July 31, 2012

    TUHUMA ZA HUJUMA ZAMUUMIZA SURE BOY


    Sure Boy Jr.

    Na Prince Akbar
    KIUNGO wa Azam FC, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, amesema kwamba anasikitishwa na tuhuma zilizozagaa kwamba yeye ni miongoni mwa wachezaji waliocheza chini ya kiwango katika Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame dhidi ya Yanga, timu yao ikilala 2-0.
    Sure Boy Jr. ameiambia BIN ZUBEIRY kwamba tuhuma hizo zinamnyima raha na kwa mara ya kwanza tangu aanze kuchezea Azam, hivi sasa anajisikia mnyonge.
    Sure amekana tuhuma hizo hazina ukweli wowote ndani yake na kwamba wanazungumza dhana tu, kitu ambacho ameonya si kizuri na kitaivuruga timu yao.
    “Ukiutazama ule mchezo, utaona sisi tulijituma sana, siwezi kusema nani hakucheza kwa uwezo wake wote, muda mwingi tulikuwa kwenye lango lao na tulitengeneza nafasi nyingi kuliko wao. Ila tu bahati haikuwa yetu.
    Kuna bao moja Yanga waliokoa mpira ukiwa unaelekea nyavuni na mimi ndiye nilitoa pasi ya mwisho, sasa unasemaje tulihujumu timu? Au kwa kuwa tumefungwa? Mimi kwa kweli sipendi haya maneno.
    Sisi tulitaka hilo Kombe, lakini bahati haikuwa yetu. Sisi ndio tumeumia zaidi. Mimi nawashauri viongozi wetu, wayachukulie haya kama matokeo ya kawaida ya mchezo, tusianze kuvurugana saa hizi mapema, tuanze kujipanga kwa ajili ya mechi ya Ngao ya Jamii na Ligi Kuu,”alisema kiungo huyo bora kwa sasa Afrika Mashariki na Kati.
    Jumamosi Azam ilifungwa mabao 2-0 na Yanga katika fainali ya Kagame, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kushindwa kutimiza ndoto zake za kuwa timu ya kwanza nje ya Simba na Yanga kutwaa Kombe hilo.
    Lakini wengi wanaamini, Sure anakuwa miongoni mwa wanaotuhumiwa kwa sababu baba yake mzazi, Abubakar Salum ni kocha wa timu ya vijana ya Yanga ni pia mchezaji wa zamani wa klabu hiyo.   

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TUHUMA ZA HUJUMA ZAMUUMIZA SURE BOY Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top