• HABARI MPYA

  Saturday, July 28, 2012

  NIZAR NJE WIKI SITA YANGA


  Nizar Khalfan

  Na Prince Akbar
  KIUNGO wa kimataifa wa Tanzania, Nizar Khalfan aliyesajiliwa na Yanga msimu huu, atakuwa nje ya Uwanja kwa wiki sita baada ya kuumia nyonga katika mfululizo wa michuano ya Klabu Bingwa ya soka Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame inayofikia tamati leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, tangu ianze Julai 14, mwaka huu.
  Kocha wa Yanga, Mbelgiji Tom Saintfiet ameiambia BIN ZUBEIRY jana kwamba Nizar alionyesha dalili za kupona mapema awali, lakini sasa imegundulika anatakiwa kuwa nje ya Uwanja kwa wiki zisizopungua sita.
  Kwa masikitiko makubwa, Tom alisema; “Nizar hatacheza fainali, alionekana kuwa vizuri siku chache zilizopita, sasa atakuwa nje kwa wiki zisizopungua sita,”alisema.
  Tayari Nizar amekosa mechi mbili za Robo Fainali na Nusu Fainali ya michuano hiyo, licha ya kuanza vizuri katika hatua ya makundi. Kiungo huyo alisajiliwa na Yanga miezi miwili iliyopita akitokea Philadelphia Union ya Ligi Kuu ya Marekani (MLS), ambayo alijiunga nayo kutoka Vancouver Whitecaps ya Canada, ambayo ilikuwa inacheza MLS.
  Maana yake, Nizar ambaye tayari ana ofa ya kwenda kucheza Qatar, atakosa hadi mechi za mwanzoni mwa msimu ujao wa Ligi Kuu ya Bara na kama Yanga itakubali kushiriki michuano mipya ya timu nane, nne za Bara na nne Visiwani, Bank ABC Super8 Tournament pia kiungo huyo hatacheza. 
  Uchunguzi unaonyesha kuumia kwa wachezaji wengi wa klabu za Tanzania mwanzoni mwa msimu kunatokana na kukosa mazoezi ya kutosha kabla ya msimu na kucheza mechi za karibu karibu- mfano za Kombe la Kagame.
  Mbali na Nizar, kwa Yanga wachezaji wengine ambao ni majeruhi ni kipa Yaw Berko na beki Juma Abdul, wakati wachezaji wengine wanaendelea kucheza wakiugulia maumivu. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NIZAR NJE WIKI SITA YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top