• HABARI MPYA

  Tuesday, July 24, 2012

  SIMBA NA AZAM UTAMU AMBAO PENGINE USIUONE TENA KAGAME HII


  Kikosi cha Azam waliosimama kutoka kulia Ibra Mwaipopo, Joseph Owino, John Bocco, Erasto Nyoni, Rama Chombo na Deo Munishi. Walioinama kutoka kulia ni Aggrey Morris, Hamisi Mcha 'Vialli', brahim Shikanda, 

  Na Princess Asia
  BINGWA wa Ligi Kuu ya Bara, Simba SC leo atakuwa na mtihani mzito mbele ya washindi wa pili wa ligi hiyo, Azam FC katika mchezo wa Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Mchezo huo wa Robo Fainali, unazikutanisha timu hizo wiki mbili tangu zikutane kwenye Fainali ya Kombe la Urafiki, ambayo Simba ilishida kwa penalti 3-1, kufuatia sare ya 2-2 ndani ya dakika 90.
  Katika mchezo huo, mshambuliaji wa kimataifa wa Zambia, Felix Sunzu alitangulia kuifungia Simba dakika ya 29 kabla ya Hamisi Mcha ‘Vialli’ kusawazisha dakika ya 45 na ushei.
  Kipindi cha pili mchezo ulichangamka zaidi na dakika ya 81, John Bocco ‘Adebayor’ aliyetokea benchi aliifungia Azam bao la pili, kabla ya Kazimoto kuisawazishia Simba kwa penalti dakika ya 87, baada ya Danny Mrwanda kuangushwa kwenye eneo la hatari.
  Penalti za Simba zilikwamishwa nyavuni na Mwinyi Kazomoto, Amir Maftah na Kiggi Makassy, wakati Haruna Moshi Boban alipaisha na kwa upande wa Azam FC, aliyefunga ni Hamisi Mcha ‘Vialli’ pekee, wakati Samir Hajji Nuhu, Ibrahim Mwaipopo na Himid Mao walikosa.
  Katika siku za karibuni, Simba na Azam zinaonekana kuchuana vikali, kwani mbali na Azam kuwa wa pili ya nyuma kwenye Kombe la Urafiki, hata kwenye Ligi Kuu walifuata hivyo hivyo
  Simba imefuzu Robo Fainali kama mshindi wa tatu kwenye Kundi A, ikivuna pointi nne, kutokana na kufungwa mechi moja (2-0 dhidi ya URA), kushinda moja dhidi ya Ports ya Djibouti na sare moja dhidi ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
  Azam yenyewe imefuzu kama kinara wa Kundi B, lakini herufi tu, kwani timu zote za Kundi hilo zililingana kwa pointi, mbili kila moja na kutokana na sare katika mechi zote (1-1 Azam na Mafunzo, 0-0 Mafunzo na Tusker, 0-0, Azam Tusker na 0-0 Mafunzo na Tusker).
  Mchezo wa leo, utatanguliwa na Robo Fainali nyingine kati ya Atletico ya Burundi AS Vita ya DRC.
  Habari za ndani kutoka Azam zinasema kwamba viongozi wa klabu hiyo wametoa angalizo kwa TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) na CECAFA (Baraza la Vyama Soka Afrika Mashariki) wanataka haki itendeke kwenye mechi hiyo.
  Kiongozi mmoja wa juu wa Azam, ambaye hakupenda kutajwa jina, alisema kuna desturi ya Simba na Yana kubebwa kwenye mashindano ili zicheze fainali na CECAFA na TFF watimize ndoto zao za kukusanya  mapato mengi milangoni, lakini wanaomba desturi hiyo leo iwekwe kando.
  “Sisi Azam tuko tayari kuaga kwenye mashindano bila ya malalamiko na kuchukua ilikuwa hali mchezo, lakini kama tutaona dalili zozote za wapinzani wetu kupendelewa, tutachukua hatua,”alisema.   
  Kikosi cha Simba waliosimama kutoka kulia Juma Kaseja, Mussa Mudde, Amri Kiemba, Lino Masombo, Felix Sunzu na Abdallah Juma. Walioinama kutoka kulia ni Shomary Kapombe, Haruna Shamte, Mwinyi Kazimoto, Juma Nyosso na Kanu Mbivayanga.

  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA NA AZAM UTAMU AMBAO PENGINE USIUONE TENA KAGAME HII Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top