• HABARI MPYA

  Sunday, July 29, 2012

  KOSA MOJA WALILOFANYA TFF BANK ABC SUPER 8 NI KUBWA SANA


  Simba SC; Imeonyesha nia ya kushiriki 


  KATIKA siku ambayo Yanga ilitinga Nusu Fainali ya Klabu Bingwa ya soka Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame nilikuwa nina mazungumzo na Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Leodegar Chillah Tenga.
  Na Mahmoud Zubeiry
  Mazungumzo yetu yalianzia Uwanja wa Taifa tukiwa kwenye gari lake kuelekea mjini na yalitosha kwa sababu ya foleni. Tulikuwa wawili tu kwenye gari na yalidumu kwa zaidi ya nusu saa tukiwa njani, kutokana na foleni.
  Tulijadili mambo kadha wa kadhaa, kwanza ni kuhusu timu zetu na wachezaji chipukizi ambao ndio taswira ya baadaye ya soka ya Tanzania. Tenga ambaye pia ni rais wa TFF, alisema amefurahishwa na wachezaji vijana wadogo waliong’ara kwenye mashindano hayo kama Said Bahanuzi ‘Spider Man’, Juma Abdul wa Yanga, Khamisi Mcha ‘Vialli’, Salum Abubakar ‘Sure Boy Jr’ wa Azam na wengineo.
  Katika timu zetu na ushiriki wao kwenye mashindano hayo, kwa pamoja tulijiridhisha, hazikuwa na maandalizi ya kutosha kabla ya mashindano na Tenga akasema ni muhimu kukawa na programu ya taifa ya maandalizi ya kabla ya msimu na akaniambia tayari amemuagiza Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Sunday Kayuni kulifanyia kazi hilo.
  Siku mbili baadaye, TFF ikatangaza mashindano mapya ya Bank ABC Super 8, ambayo yamepangwa kuanza Agosti 4 hadi 18, mwaka huu yakishirikisha timu nane, nne za Zanzibar na nne za Bara.
  Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alisema kwamba timu tatu zilizoshika nafasi za juu katika Ligi Kuu zote mbili zitaingia moja kwa moja, wakati timu moja kila upande iliyoongoza katika kampeni ya kupanda Ligi Kuu, zitashirikishwa pia.
  Alisema timu hizo zitakuwa katika makundi mawili na hakutakuwa na mechi ya kusaka mshindi wa tatu zaidi ya kuwepo kwa zawadi kwa timu itakayotwaa ubingwa tu na tayari wameshaziandikia barua za kuzitaarifu kuhusiana na michuano hiyo.
  “Nadhani hii ni nafasi nyingine kwa timu kuonyesha ushindani katika michuano hii, pia pamoja na kujiandaa kwa msimu mpya wa ligi, makocha wa timu shiriki wataweza kujua kiwango kilichopo kwenye timu zao na kama kuna kasoro warekebishe kabla ya kuanza kwa ligi,”alisema.
  Bank ABC ambayo imedhamini michuano hiyo kwa miaka mitatu, kupitia kwa Mkurugenzi wake Mkuu Boni Nyoni alisema wameamua kuandaa michuano hiyo ili kuunga mkono jitihada za maendeleo ya soka hapa nchini.

  HONGERA TFF KWA MICHUANO HII…
  Moja ya sababu za wachezaji wetu kutokuwa fiti kwa angalau asilimia 70, ni kutokana na kukosa mechi za kutosha za ushindani, kwani wengi wao zaidi ya Ligi Kuu hawana sehemu nyingine ya kuongeza uzoefu wao kiuchezaji.
  Kwa hivyo ujio wa mashindano kama haya, ambayo dhahiri yatakuwa ya ushindani ni jambo la kufurahia na kwa sababu hiyo hatuna budi kuipongeza TFF na kuiomba itanue zaidi wigo wa kutafuta udhamini kwa ajili ya mashindano mengine muhimu.
  Muda mrefu sijamuona Mkurugenzi wa Masoko wa TFF, Jimmy Kabwe akijitokeza kifua mbele, kwa sababu vyombo vya habari vimekuwa vikimnyooshea sana vidole juu ya utendaji wake, kiasi cha kutilia shaka uwezo wake na uzoefu katika jukumu alilopewa.
  Zaidi ya kumuona katika utiaji saini wa mkataba wa udhamini wa timu ya taifa, Taifa Stars na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), ndio nilimuona tena nyota huyo wa filamu ya Secret katika kutangazwa kwa Super 8 ya Bank ABC.
  Nampongeza Jimmy na sasa aelewe kama atatekeleza wajibu wake vizuri, baadala ya kukaa mezani na kuchati kwenye tweetter na facebook, kila mmoja atakuwa rafiki yake, kwani shida yetu ni kuona ufanisi.
  Kwa sasa tunaona kabisa shirikisho linakabiliwa na mzigo mzito- mashindano ya Kombe la FA hayapo, yanataka kurudi ha hayana udhamini hadi sasa, tunahitaji kuwa na Ligi madhubuti ya timu za vijana za klabu za Ligi Kuu, lakini bila udhamini haiwezekani.
  Timu zetu zote za taifa hazina udhamini, ukiondoa ule wa timu ya wakubwa. Bado soka haitumiki ipasavyo hapa nchini katika kampeni za kibiashara kama ilivyo nchi za wenzetu- tunataka kuona wachezaji wa timu ya taifa wanaingia mikataba mikubwa ya madau makubwa ya matangazo ya biashara. Kwa kweli Jimmy anatakiwa kujua, ana kazi kubwa bado ya kufanya ili kutimiza wajibu wake vema.

  MICHUANO HII IMEKUJA WAKATI SIYO…   
  Ingawa ujio wa michuano hii ni habari njema kwa soka ya Tanzania, lakini kwa sababu moja au mbili, imepokewa vibaya na klabu nchini.
  Kocha wa Yanga, Tom Saintfiet raia wa Ubelgiji alikuwa wa kwanza kuonyesha hayuko tayari kuingiza timu yake kwenye michuano hiyo kwa sababu anaamini itawaumiza wachezaji wake.
  Alisema kwamba baada ya mashindano ya Klabu Bingwa ya soka Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame jana klabu yake ikitetea taji, ni vema wachezaji wakapewa muda wa kupumzika, badala ya kupewa adhabu nyingine.
  “Tunahitaji kupumzika, tunawaumiza wachezaji wetu, bado sijaambiwa rasmi, nimekamilisha programu yangu ya mazoezi(ya Kagame) na baada ya mechi na Azam, lazima wachezaji wangu wapumzike hadi Alhamisi. Ijumaa (Agosti 3) tunaanza upya programu ya mazoezi kwa ajili ya Ligi Kuu,”alisema Saintfiet.
  Wakati kocha wa Yanga, washindi wa tatu wa Ligi Kuu ya Bara, Mtakatifu Tom akitoa msimamo huo, BIN ZUBEIRY inafahamu mabingwa wa Ligi Kuu ya Bara, Simba SC, baada ya kutolewa wamewapa mapumziko wachezaji wake na watakutana wiki ijayo kuanza maandalizi ya tamasha lao la kila mwaka, Simba Day, litakalofanyika Agosti 8, mwaka huu na tayari wamekwishatoa ratiba yao kuanzia Agosti 5 hadi 11, mwaka huu. 
  Agosti 5, Simba itakuwa na Mkutano Mkuu wa mwaka katika ukumbi wa Polisi Oystrebay na siku hiyo hiyo watazindua Wiki ya Simba na Jamii, kuelekea Simba Day Agosti 6, watatembelea watoto yatima katika kituo cha Maungu Orphanage, Kinondoni Mkwajuni, Agosti 7, watatembelea wagonjwa katika hospitali ya Mwananyamala na Agosti 8, watafanya tamasha la Simba Day Uwanja wa Taifa, likitanguliwa na burudani kadhaa kabla ya mechi dhidi ya klabu moja kubwa barani.
  Agosti 9, Simba watatembelea shule ya msingi Mgulani kuhamasisha michezo mashuleni na Agosti 10, watatembelea kiwanda cha Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) Ilala, ambao ni wadhamini wao wakuu, kupitia bia ya Kilimanjaro Premium Lager.
  Tayari wadhamini wakuu wa Simba SC, kupitia Meneja wa bia ya Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe wamekwishakabidhi fedha, Sh. Milioni 20 kwa ajili ya Mkutano Mkuu na fedha nyingine za tamasha zitatolewa wiki ijayo.
  Na jana Mwenyekiti wa Simba, Alhaj Ismail Aden Rage alisema atakuwa tayari kuiruhusu timu yake kushiriki mashindano hayo, iwapo Simba wataonyeshwa mikataba ya mashindano hayo ambayo TFF wameingia na wadhamini, Bank ABC.
  Hapa Rage yupo kimaslahi zaidi na si kuhusu mustakabali wa timu. Mara baada ya Simba kutolewa na Azam katika Kombe la Kagame, Kocha Milovan Cirkovick alisema aliwaambia mapema viongozi wake kwamba timu haina maandalizi ya kutosha na hakutaka iingie kwenye mashindano hayo, ila viongozi wakalazimisha.
  Sasa katika kipindi hiki ambacho Milo yuko kwa Serbia kwa mapumziko ya wiki moja, akirudi tu atafikia michuano hiyo, je saa ngapi atakuwa amewaandaa wachezaji wake?
  Ni kweli Rage alishauriana na kocha Milovan kabla ya kutoa tamko lake? Sijui, lakini nasema soka ya Tanzania kwa aina ya viongozi tulionao, tuna safari ndefu sana kufikia mafanikio. Sasa huyu ndiye Rage, ambaye angalau kidogo ameucheza mpira, ana uzoefu wa uongozi wa soka na hata kielimu si haba- Mhasibu huyo bwana, je wale wenzangu na mie akina Iddi Godi Godi tutarajie nini kutoka kwao?    
  Azam kama klabu, hawajatoa tamko rasmi, lakini wachezaji wake wamesema wanataka kupumzika na hawako tayari kucheza michuano ya Bank ABC Super 8 na wamependekeza labda, wacheze wachezaji wa timu ya Academy michuano hiyo.
  Wakizungumza na BIN ZUBEIRY kwa masharti ya kutotajwa majina yao kukwepa kuingilia uhuru wa viongozi, wachezaji hao walisema kwamba tangu kumalizika kwa Ligi Kuu Aprili mwaka huu hawajapumzika, hivyo wanataka kupumzika japo kwa wiki moja kabla ya kuanza rasmi kwa msimu mpya.
  “Ligi imeisha tumengia kwenye kambi ya timu ya taifa, tumecheza na Ivory Coast, tumecheza na Gambia, tumecheza na Msumbiji na baada ya hapo tumerudi hapa, tunaingia kwenye Kombe la Urafiki. Tunatoka huko, tunaingia moja kwa moja kwenye Kombe la Kagame, jamani tena tutoke hapa tuingie kwenye mashindano mengine! Na sisi ni binadamu jamani,”alisema mchezaji mmoja wa klabu hiyo tegemeo.
  Lakini pia, BIN ZUBEIRY inatambua Azam ambao ni washindi wa pili wa ligi hiyo, Azam watakuwa na ziara ya wiki mbili nje ya nchi kujiandaa na msimu mpya.

  MASHINDANO HAYA YAFANYIKE DESEMBA
  Tumeuona ugumu wa mashindano haya kufanyika mwezi ujao na kama TFF itataka kulazimisha, lazima wajue kabisa hatutakuwa na mashindano bora na hayatakuwa na tija.
  Timu tatu za Bara, Simba mabingwa, Azam washindi wa pili na Yanga wa tatu wametoka kwenye Kombe la Kagame wamechoka na wachezaji wao wengi wameumia kwenye mashindano hayo, kutokana na kuingia kwenye michuano hiyo wakiwa hawako fiti kimazoezi.
  Tenga amecheza mpira, atakuwa anajua. Hata Angetile huwa anasema alicheza na marehemu Saidi Mwamba Kizota huko Tabora, basi atakuwa anajua pia- lakini Sunday Kayuni ni mwalimu anajua nina hakika na kwa kuwa ninamjua ni mtu wa misimamo sijui ingekuwaje kama yeye ndiye angekuwa kocha wa Simba, halafu TFF inataka kumburuza namna hii.
  Kosa moja kubwa ambalo TFF wamefanya ni kutozishirikisha klabu katika mjadala wa ujio wa mashindano haya, kwani kama wangewashirikisha basi, leo kauli zisingepishana. Wote wangeongea lugha moja. Na ndiyo maana kuna wakati huwa namstaajabu sana Angetile, anakuwa kama mtu ambaye hajatokea newsroom.
  TFF wanawezaje kukaa na kuamua hadi kupanga bila kuwasiliana na wadau, klabu ambao wao ndio wanacheza mashindano hayo? Hii haijakaa sawa na huko tunapoelekea, lazima Angetile abadilike, maana anaonekana siku hizi hata sura yake, amekuwa mchungu mno na japokuwa hajasema, lakini inaonekana sasa anachukia sana Waandishi wenzake, tena kuliko Rage alivyokuwa anamchukia yeye enzi zake Nipashe.
  Mimi nawashauri TFF, waanze upya taratibu za mashindano haya, wakutane na klabu, wawaonyeshe hiyo mikataba na wapange tarahe mpya ya mashindano yenyewe.
  Ligi yetu inaanza mwezi ujao na Novemba tutamaliza mzunguko wa kwanza- Desemba kutakuwa kuna Kombe la Challenge kabla ya kurejea kwa Ligi Kuu Januari na Februari klabu nne kati ya nane zinazotarajiwa kushiriki mashindano hayo zitaingia kwenye michuano ya Afrika.
  Sasa tuangalie kuanzia Desemba, wapi tuyachomeke mashindano haya, ili yawe na maana halisi ya maandalizi ya msimu mpya. Maana japokuwa sisi ligi yetu inaanza Agosti, lakini utaona tunahitaji kuwekeza zaidi katika maandalizi ya mwishoni mwa mwaka, kwa sababu ndio tunaelekea kwenye mashindano makubwa, yakiwemo ya Afrika na lala salama ya Ligi Kuu.
  Nimalizie tu kwa kuwapongeza tena TFF na hasa Mkurugenzi wa Masoko bwana Jimmy Kabwe kwa kutuletea Super 8 ya Bank ABC, ila tu nawaambia kosa moja walilofanya ni kubwa sana. Warekebishe, mambo yaende sawa. Ramadhan Karim.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KOSA MOJA WALILOFANYA TFF BANK ABC SUPER 8 NI KUBWA SANA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top