• HABARI MPYA

  Friday, July 20, 2012

  HIZI NI SALAMU ZANGU KWENU WANA SIMBA, WAJUAJI WANAHARIBU TIMU YENU


  Na Mahmoud Zubeiry

  KUNA mawazo potofu ndani ya Simba na sijui yanatokea wapi. Mawazo potofu, ambayo kama yataachwa yaendelee kufanya kazi yatazidi kuivuruga klabu hiyo.
  Hivi sasa kuna kampeni ya ‘Simba haina washambuliaji’ inaendelea, ambayo unaweza kuona lengo lake ni kuwapiga zengwe washambuliaji waliopo. Na ukiitazama kwa kina, unaweza kuona kuna mtu ndani ya Simba, kwa ubinfasi wake hamtaki mshambuliaji Abdallah Juma, ambaye tayari amekwishawadhihirishia wana Simba ana uwezo.
  Kuna mtu anaaminiwa na kuogopgwa hata na viongozi wakuu ndani ya Simba SC, kiasi huyo sasa ndiye unaweza kumuita mwenye Simba yake. Naye hutamba hivyo; “Timu yangu….”. kosa kubwa, Simba siyo timu ya mtu, ni timu ya watu.
  Mapema tu Abdallah Juma aliposajiliwa chombo kimoja cha habari kikamkandia Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ kwamba kajiamulia mwenyewe kumsajili mshambuliaji huyo kutoka Ruvu Shooting, bila kushirikisha Kamati ya Utendaji.
  Dullah Mabao
  Na kwa kudhihirisha mtu huyo anaogopwa na hadi viongozi wakuu wa Simba, ilibidi Kaburu ajitetee kwamba mchezaji huyo hajasajiliwa, bali ameenda kufanya majaribio. Inasikitisha kuona kwamba hadi dunia ya leo Miungo watu bado wapo!  
  Kampeni za kumpinga mshambuliaji huyo zimeendelea na unaweza kujionea pamoja na kuanza kufanya vizuri tangu kwenye mechi za kirafiki, lakini bado imekuwa vigumu kwake kuaminiwa katika kikosi cha kwanza.
  Sitaki kuamini haya ni mawazo ya Profesa Milovan Cirkovick- naamini ni shinikizo kutoka nje ya benchi la ufundi.
  Real Madrid leo wanakwenda mbio kuwania saini ya Luca Modric kutoka Tottenham Hotspur, lakini huwezi kujua ni chaguo la nani kati ya kocha Jose Mourinho na rais Florentino Perez- hivyo haiwezi kuwa ajabu hata Tanzania, Makamu wa Rais wa Simba akisajili.
  Hadi wanachama kufikia kumpa kura za kutosha Kaburu kuwa Makamu wao, walimuamini kwamba ni mtu wa mpira na wakampa dhamana- hivyo yeye kusajili si kosa.
  Na pia mtu anayeweza kuidhinisha au kukwamisha usajili wa mchezaji ni mwalimu na si Kamati ya Ufundi wala ya Utendaji, labda kuwe kuna sababu nyingine nje ya mpira.
  Lakini kwa nini basi tusikubali amefanya ubinfasi wenye manufaa, kwa kusajili mchezaji mzuri ambaye leo anaelekea kuwa kinara wa mabao wa timu?
  Namfahamu Salim Kinje, mwaka 1999 alikuwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20 pamoja na akina Jemedari Said, Yahya Issa, Simon Butte na wengineo, ambao hivi sasa wamekwishatundika daluga wote.
  Nani kamsajili huyu Simba, ni Kaburu au Milovan? Akina Juma Kaseja, Haruna Moshi ‘Boban’, ambao hivi sasa wanaitwa ‘wazee’ waliibukia kwenye kikosi cha timu ya vijana chini ya umri wa miaka 17, mwaka 2000 chini ya makocha Ernest Mokake na Juma Matokeo, ambao wote hivi sasa ni marehemu.  
  Kikosi cha Simba 2012, kutoka kushoto Felix Sunzu, Lino Masombo, Amri Kiemba, Amir Maftah, Kanu Mbivayanga, Shomary Kapombe, Haruna Sgamte, Mwinyi Kazimoto, Haruna Moshi na Mussa Mudde, wakati mbele yao ni Nahodha Juma Kaseja. Hiki si kikosi cha mzaha kama kinapata muda wa kutosha wa maandalizi.
  Tazama Simba inavyojikwaa na kesho wasije kujiuliza walinguka kwa sababu gani. Mawazo potofu ndani ya Simba yalisababisha akaachwa beki Haruna Shamte na kiungo Amri Kiemba, ambao unaweza kuona wanacheza vizuri kikosini hivi sasa, baada ya kurejeshwa kwa shinikizo la kocha.
  Sijui haya mawazo potofu yanatoka wapi, lakini kwa haraka naweza kusema udhaifu unaanzia kwenye Kamati ya Utendaji chini ya Mwenyekiti Alhaj Ismail Aden Rage, kuwapa watu majukumu mazito kuliko uwezo wao.
  Ibrahim Masoud ‘Maesrto’ ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Simba SC; huu ni mzaha. Simba imeishiwa kiasi gani hadi kuwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi aina ya huyu?
  Hii ni klabu kubwa yenye wachezaji wengi wastaafu wenye taaluma ya ukocha na wazoefu, weledi wa masuala ya soka-  lakini kwa kile ambacho nakiita udhaifu unaoanzia kwenye Kamati ya Utendaji ndio chanzo cha yote haya.
  Ndiyo maana sasa anasimama mtu anasema Simba ina tatizo la washambuliaji, kisa imewafunga vibonde Ports ya Sudan mabao matatu tu, lakini mtu huyu anashindwa kuurejea mchezo ulivyokuwa na kujiuliza timu ilitengeneza nafasi ngapi za kufunga mabao na ikatumia ngapi?
  Miguuni mwa Felix Sunzu pekee, Simba ilipoteza mabao sita ya wazi, kama angefunga angalau matatu- ingekuwaje? Dullah Mabao pamoja na kufunga mara mbili, lakini alikosa bao moja la wazi sana kipindi cha pili. Na hapa tunaiweka wapi kauli ya wenye soka yao, Football is the game of chance?
  Tunapenda kufanya mambo kwa mazoea, kwa sababu Ports ilifungwa saba na AS Vita, basi Simba nayo ilistahili kushinda saba- hapana soka haiko hivyo.
  Juni 1, mwaka 2002, Ujerumani iliitandika Saudi Arabia mabao 8-0 katika Fainali za Kombe la Dunia, Korea Kusini na Japan, lakini Cameroon iliyoonekana kutopishana sana makali na Wajerumani, tena wakiongozwa na Samuel Eto’o bado kijana mdogo, walishinda 1-0 kwa mbinde. Hii ndiyo soka.
  Lakini kwa nini uwadanganye wana Simba timu ina tatizo la washambuliaji wakati kuna Felix Sunzu, Danny Mrwanda, Haruna Moshi na Dullah Mabao?
  Mfumo unaotawala katika dunia ya soka ya leo ni kutumia viungo wengi na mshambuliaji sana mmoja tu- je hadi hapa bado unaweza kusema Simba ina washambuliaji wachache?
  Simba ina viungo wa kutosha kabisa, akina Uhuru Suleiman, Mussa Mudde, Kanu Mbivayanga, ‘Babu’ Kinje, Kiggi Makassy, Christopher Edward, Mwinyi Kazimoto, Jonas Mkude, Amri Kiemba na sijui nimemsahau nani hapa. Bado Emmanuel Okwi yuko mguu nje ndani, anaweza kufeli majaribio (simuombei hivyo) na akarudi Simba kama alivyoahidi.
  Mwenyekiti wa Simba Alhaj Ismail Aden Rage kulia, akishuhudia kocha Milovan Cirkovick anavyosaini mkataba mwaka jana, kushoto ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Simba SC, Ibrahim Masoud 'Maestro'. 

  NINI TATIZO LA SIMBA?
  Alichosema Milovan kwenye Mkutano na Waandishi wa Habari leo, kwamba timu bado ni mpya wachezaji hawajazoeana ndicho ambacho hata mimi naunga mkono. Matatizo madogo madogo ya kufunga mabao yataisha timu itakapozoeana.
  Soka ina wigo mpana sana na inahitaji muda wa kutosha kujifunza kabla ya kuanza kujiona wajuaji, kisa tu tunapewa pewa nafasi ya kuandika andika kwenye kurasa za magazeti au kuzungumza kwenye vipindi vya Radio na Televisheni. Hapana.
  Mshauri wa Ufundi wa Enyimba FC International anaitwa Abdu Maikaba, ambaye wakati fulani mwaka jana alikuwa kocha wa muda wa timu, baada ya kufukuzwa kwa Evans Ogenyi kutokana na matokeo mabaya.
  Huyu jamaa ana umri wa miaka 46, alizaliwa mwaka 1965, na alianza ukocha katika klabu ya Kano Pillars, kabla ya kwenda Buffalo FC, badaaye,  FC Abuja alikokuwa Kocha Mkuu hadi anaingia Enyimba mwaka 2009, kwanza kama kocha Msaidizi.
  Naomba wasifu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Simba SC, halafu niambie kwa nini asiwe Zamoyoni Mogella, Khalid Abeid, au Abdallah ‘King’ Kibadeni, aliyeitwa Chifu Mputa Songea?
  Namaliza kwa kuweka msistizo, Simba haina tatizo la washambuliaji, bali timu haijakaa sawa na inahitaji muda wa kutosha wa maandalizi. Hizi ni salamu zangu kwa wana Simba wote. Alamsiki.
  Danny Mrwanda, mshambuliaji hatari hadi taifa linajua, unasemaje Simba haina washambuliaji? 

  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: HIZI NI SALAMU ZANGU KWENU WANA SIMBA, WAJUAJI WANAHARIBU TIMU YENU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top