• HABARI MPYA

  Friday, July 27, 2012

  KOCHA AZAM AWEKA MSISTIZO; KIVYOVYOTE NATAKA KOMBE


  Stewart Hall

  Na Prince Akbar
  KOCHA wa Azam FC, Muingereza Stewart Hall amesema kwamba Yanga ni timu nzuri na fainali ya Klabu Bingwa ya soka Africa Mashariki na Kati itakuwa ‘classic’, yaani baab kubwa kesho Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Stewart ambaye mapema mwaka huu aliiwezesha Azam kutwaa taji la kwanza, Kombe la Mapinduzi, alisema kwamba Yanga imekuwa ikiimarika siku hadi siku na sasa imefikia kuwa timu bora na anatarajia upinzani mkali kesho.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY baada ya mechi za Nusu Fainali jana, Muingereza huyo alisema kwamba pamoja na ukweli huo nia yao Azam ni kutwaa Kombe hilo.
  “Vijana wangu hadi sasa wamenifurahisha kwa kucheza kwa kufuata maelekezo yangu. Mechi na AS Vita ilikuwa ngumu, hadi mapumziko tulikuwa nyuma kwa 1-0. Lakini niliwaambia tukiwa vyumbani, watulie tuendelee kucheza mpira wetu, tusihamaki, walinielewa na wakacheza nilivyotaka.
  Hiyo ndio siri ya ushindi, kwa kiwango kile na uchezaji ule, naona kabisa tunaweza kuwafunga Yanga na kuchukua Kombe, timu yetu ni nzuri na wachezaji wanatulia uwanjani kama ulivyoona,”alisema.
  Stewart aliiwezesha Azam kuwa timu ya pili nje ya Simba na Yanga kuingia fainali ya Kombe la Kagame, baada ya Moro United mwaka 2006, ambayo ilifungwa na Polisi Uganda mabao 2-1.
  Siku hiyo, rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwa hajatimiza mwaka tangu aanze kuishi Ikulu, alikuwepo uwanjani na aliinuka kushangilia bao la kwanza lililoelekea kubakiza Kombe nyumbani, ambalo lilifungwa na winga Julius Mrope, hata hivyo Polisi ikifundishwa na Sam Timbe wakati huo, ilitoka nyuma na kushinda 2-1.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KOCHA AZAM AWEKA MSISTIZO; KIVYOVYOTE NATAKA KOMBE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top