• HABARI MPYA

    Tuesday, July 31, 2012

    NGORONGORO, FLYING EAGLES WAINGIZA MILIONI 12


    Katibu wa TFF, Angetile Osiah, kulia na Ofisa Habari wa TFF, Boniphace Wambura kushoto wakizungumza na Waandishi wa Habari, ofisi za TFF, Ilala, Dar es Salaam mchana wa leo.

    Na Princess Asia
    MECHI ya kwanza ya raundi ya pili kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 20 kati ya Tanzania (Ngorongoro Heroes) na Nigeria (Flying Eagles) iliyochezwa juzi (Julai 29 mwaka huu) imeingiza sh. 12,901,000.
    Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniphace Wambura Mgoyo ameiambia BIN ZUBEIRY mchana huu kwamba, fedha hizo zimepatikana kutokana na watazamaji 3,377 waliokata tiketi kushuhudia pambano hilo lililochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Alisema sehemu iliyoingiza watazamaji wengi ilikuwa viti vya bluu na kijani ambapo 2,697 walikata tiketi kwa kiingilio cha sh. 3,000 kila mmoja. Viingilio vingine katika mechi hiyo vilikuwa sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, sh. 10,000 kwa VIP C na B, na sh. 15,000 kwa VIP A iliyoingiza watazamaji 21.
    Alisema mgawanyo wa mapato hayo ni kama ifuatavyo; asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ilikuwa sh. 1,967,949.15, gharama ya kuchapa tiketi sh. 2,250,000, gharama za waamuzi na kamishna wa mechi hiyo sh. 760,000 na ulinzi na usafi kwa Uwanja wa Taifa sh. 2,350,000.
    Alisema malipo kwa Wachina (Beijing Construction) sh. 2,000,000, asilimia 20 ya gharama za mchezo ni sh. 714,610.17, asilimia 10 ya uwanja sh. 357,305.08, asilimia 5 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) sh. 178,652.54 na asilimia 65 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) sh. 2,322,483.05.
    Mechi ya marudiano ya michuano hiyo ambayo fainali zake zitafanyika mwakani nchini Algeria itachezwa Agosti 12 mwaka mjini Ilorin, Jimbo la Kwara, Nigeria.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NGORONGORO, FLYING EAGLES WAINGIZA MILIONI 12 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top