• HABARI MPYA

    Sunday, July 29, 2012

    'SUPER EAGLES' WAITUNDIKA 2-1 NGORONGORO


    Ngorongoro wakitoka uwanjani vichwa chini

    Na Prince Akbar
    TIMU ya soka ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro Heroes leo imeanza vibaya kampeni za kuwania kucheza Fainali za Afrika kwa vijana wenye umri huo, zitakazofanyika nchini Algeria mwakani, baada ya kufungwa na Nigeria mabao 2-1, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Achaji Gero; Aliyefunga mabao yote ya Nigeria
    Hadi mapumziko, Nigeria, Flying Eagles walioonekana kutumia wachezaji waliozidi umri, walikuwa mbele kwa mbele kwa mabao 2-0 katika mchezo huo wa kwanza wa Raundi ya pili, yote yakitiwa kimiani na mshambuliaji wa Enugu Rangers, Achaji Gero katika dakika ya pili na 44.
    Kipindi cha pili, Ngorongoro walibadilika na kucheza vizuri, wakiwazidi wapinzani wao kumiliki mpira na kasi ya mchezo na hatimaye wakafanikiwa kupata bao la kufutia machozi, lililofungwa na Atupele Green dakika ya 50, akimalizia krosi ya Ramadhani Singano ‘Messi’.
    Ngorongoro wangeweza kupata mabao zaidi, kama wangecheza soka ya chini, lakini kutia krosi za juu kwenye lango la Nigeria ilikuwa ni kuwatesa washambuliaji wao wafupi, Atupele na Simon Msuva.
    Kwa matokeo hayo sasa, Ngorongoro wanahitaji ushindi wa angalau wa mabao 2-0 katika mchezo wa marudiano Nigeria wiki mbili zijazo, ili kusonga mbele.
    Kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen
    Baada ya mchezo huo, kocha wa Ngorongoro Heroes, Mdenmark Jakob Michelsen alisema kwamba ataongeza nguvu katika kikosi chake kwa kuwaita wachezaji wawili wanaocheza nje, kiungo Adam Nditi wa Chelsea na Thomas Ulimwengu wa Tout Puissant Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), sambamba na nyota wengine waliokwenda Ujerumani n TSU kwenye michuano ya Fallerhof.
    Huu unakuwa mchezo wa tatu mfululizo Ngorongoro inafungwa nyumbani tangu Michelsen apewe timu hiyo akirithi mikoba ya Kim Poulsen, ambaye amepandishwa timu ya wakubwa, Taifa Stars.
    Awali, Ngorongoro walifungwa mechi mbili za kirafiki na Rwanda mwezi huu, moja Chamazi 2-0 na nyingine Taifa, 2-1.
    Katika mchezo, kikosi cha Ngorongoro kilikuwa; Barwany Khomein, Omega Seme, Jamal Mroki, Issa Rashid, Ruhana Samir, Yarouk Ramadhan, Kheri Salum/Jerome Lambele, Frank Damayo, Simon Msuva, Atupele Green na Ramadhan Singano.
    Flying Eagles; Samuel Okani, Hassan Abubakar, Ahiyu Mohamed, Ikechukwu Okine, Chizoba Amaefule, Agboyi Oubokha, Moses Orkuma, Chidi Osochukwu, Yahaya Adam/Harrison Egbune, Achaji Gero na Aminu Omar/Uchw Agbo. 
    Simon Msuva akitafuta mbonu za kuwatoka mabeki wa Nigeria, 

    Atupele Green kulia akimtia kashikashi kipa wa Nigeria, Samuel Okani

    WADAU WA KWELI WA SOKA HAWACHAGUI MECHI; Nassor Bin Slum akiwa na mwanawe uwanjani

    INATAKA MOYO KUAMINI; Eti hawa U20


    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: 'SUPER EAGLES' WAITUNDIKA 2-1 NGORONGORO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top