• HABARI MPYA

  Tuesday, July 31, 2012

  NGASSA: NINGEANZA, NINGEWAFUNGA YANGA


  Ngassa

  Na Prince Akbar
  MSHAMBULIAJI wa Azam FC, Mrisho Khalfan Ngassa, amesema kwamba kama angepewa nafasi tangu mwanzo wa mchezo kwenye mechi dhidi ya Yanga, fainali ya Kombe la Kagame, Klabu Bingwa ya soka Afrika Mashariki na Kati, angeweza kufunga.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana, Ngassa alisema kwamba katika mchezo huo, aliingia wakati Yanga tayari wanaongoza bao 1-0 na wamekwishajidhatiti kulinda bao lao, hivyo jitihada zake za kuitafutia mabao timu yake, hazikuzaa matunda.
  Lakini Ngassa anaamini kama angekuwamo kwenye 11 walioanza asingetoka kapa uwanjani siku hiyo.
  “Naamini kwa asilimia 100, siku hiyo mimi ningeanza sidhani kama zile dakika 45 tu za kipindi cha kwanza zingeisha mimi sijafunga, ila naheshimu maamuzi ya kocha na nitaendelea kufuata mwongozo wake,”alisema Ngassa.
  Mfungaji huyo bora wa zamani wa Ligi Kuu, alisema kwamba baada ya kufunga bao la ushindi katika Nusu Fainali ya michuano hiyo, dhidi ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Azam ikishinda 2-1, aliamini kwenye Fainali ataanza.
  “Nilijiamini sana kwamba nitaanza, nikaenda hadi kunyoa mnyoo wenye maandishi ya jina la Azam. Nilipania kabisa niwaadhibu Yanga, lakini katika 11 walioanza sikuwemo, nikainuliwa baadaye kabisa tumekwishafungwa na mechi imekwishakuwa ngumu, ila pamoja na hayo kama watu walitazama waliona nilivyojituma,”alisema Ngassa.
  Alipoulizwa kuhusu tuhuma zinazozungumzwa kwamba alicheza kinazi kuibeba timu yake ya zamani, Ngassa alisema; “Mimi nazisikia, ila nashangaa sana, haya, mechi ya Yanga tumefungwa kwa sababu tumehujumu, na mechi na Simba fainali ya Urafiki nayo vipi, kwa nini tulifungwa?”alihoji Ngassa.
  Mrisho ametahadharisha viongozi wa Azam watazame kwanza sababu za kiufundi baada ya mchezo zitasaidia timu kurekebisha makosa, kuliko kuanza kutafutana uchawi. “Sisi ni Azam, haya mambo tuwaachie wenyewe Simba na Yanga, ndio wakifungwa tu wamehujumiwa,”alisema.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NGASSA: NINGEANZA, NINGEWAFUNGA YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top