• HABARI MPYA

    Sunday, July 22, 2012

    SPIDER MAN HATARINI KUWAKOSA MAFUNZO, NIZAR HATA JEZI HAVAI KESHO, BERKO, CHUJI, KIIZA NAO NJE NDANI


    Said Bahanuzi 'Spider Man'

    Na Prince Akbar
    MSHAMBULIAJI tegemeo wa Yanga, Said Bahanuzi ‘Spider Man’ yuko hatarini kuikosa mechi ya Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame kesho dhidi ya Mafunzo ya Zanzibar, kutokana na maumivu ya mgongo, wakat kiungo Nizar Khalfan yeye kwa asilimia 100 hatacheza kutokana na maumivu ya nyonga.
    Kocha wa Yanga, Mbelgiji Tom Saintfiet ameiambia BIN ZUBEIRY mchana huu kwamba, Nizar hatacheza kabisa, lakini wachezaji wengine watatu, Bahanuzi,  kipa Yaw Berko anayesumbuliwa na goti, kiungo Athumani Iddi ‘Chuji’ na Hamisi Kiiza wanaosumbuliwa na quadriceps wako kwenye hatihati kucheza.
    Mtakatifu Tom amesema kwamba, Daktari wa Yanga, Sufiani Juma anaendelea kufuatilia afya za Bahanuzi, Kiiza, Berko na Chuji ili kuhakikisha wanakuwa fiti kwa ajili ya mechi ya kesho, lakini kwa Nizar kocha huyo wa zamani wa Namibia na Ethiopia, amekwishakata tamaa kumtumia kwenye mechi na Mafunzo.
    Amesema sababu ya wachezaji wake kuumia mara kwa mara ni kutokana na kucheza mechi mfululizo na kulingana na kanuni za mashindano hayo, hawezi kutumia wachezaji zaidi ya 20, hivyo hana namna nyingine zaidi ya kupambana na hali hiyo.
    Bahanuzi ndiye kinara wa mabao wa Yanga hivi sasa, hadi sasa akiwa amekwishaifungia timu hiyo mabao manne, hivyo kuingia kwenye mbio za kuwania kiatu cha dhahabu cha mashindano hayo, ambayo tayari kwenye kabati la Yanga kuna mataji manne yamehifadhiwa.
    Mshambuliaji huyo mpya kutoka Mtibwa Sugar ya Morogoro, juzi alikaribia kuondoka na mpira uwanjani, kama si refa Dennis Batte kutoka Uganda kukataa bao lake moja siku ambayo alifunga mawili yaliyokubaliwa dhidi ya APR ya Rwanda, Yanga ikishinda 2-0, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jioni hii.
    Katika mchezo huo, Kocha Tom alimpumzisha Bahanuzi dakika ya 72 na nafasi yake ikachukuliwa na Jerry Tegete, wakati Nizar Khalfan kabla ya hapo alimpisha Juma Seif ‘Kijiko’.
    Wakati huo huo: Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), leo limesema kwamba mechi ya Yanga kesho itakuwa ya pili, kama ambavyo itakuwa kwa Simba keshokutwa.

    RATIBA ROBO FAINALI
    Julai 23, 2012
    URA vs APR (Saa 8:00 mchana)
    Mafunzo vs Yanga (Saa 10:00 jioni)
    Julai 24, July
    Atletico vs AS Vita (Saa 8:00 mchana)
    Azam vs Simba SC (Saa 10:000 jioni)
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SPIDER MAN HATARINI KUWAKOSA MAFUNZO, NIZAR HATA JEZI HAVAI KESHO, BERKO, CHUJI, KIIZA NAO NJE NDANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top